Wednesday, February 17, 2016

MWAMBUNGU: WATUMISHI WANAOJIHUSISHA NA VITENDO VYA WIZI WACHUKULIWE HATUA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amewataka Wakurugenzi wote katika Halmashauri  za wilaya, miji na manispaa mkoani humo kuwabana na kuwachukulia hatua za kinidhamu sambamba na kuwapeleka Mahakamani watumishi wa serikali wanaojihusisha na vitendo vya wizi, ambao wanashirikiana na wakandarasi kuhujumu miradi ya maendeleo ya wananchi kwa namna moja au nyingine.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa, amewaonya watumishi wenye tabia hiyo na kueleza kwamba wakae chonjo kwani siku zao zinahesabika, vinginevyo wanapaswa tabia hiyo kuiacha mara moja ili wasiweze kujiingiza katika mikono ya sheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani au kufukuzwa kazi.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu.
Mwambungu alisema hayo alipokuwa akitoa salamu za serikali,  kwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini katika kikao cha kupitisha rasimu ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, kilichofanyika juzi mjini hapa.

Alifafanua kuwa uaminifu na uadilifu kwa watumishi wa umma, ni jambo la lazima na siyo hiari kwa sababu serikali imewaamini na kuwapa dhamana ya kusimamia mali na fedha za wananchi, hivyo hawana mamlaka ya  kutumia fedha na madaraka yao kwa kujilimbikizia mali wao binafsi huku wakipuuza kutekeleza majukumu ya wananchi.


“Ndugu zangu kama kuna mtumishi ambaye anaona hawezi kuacha  vitendo vya wizi, atafute kazi nyingine ya kufanya serikali hii haitaweza kumvumilia mtu wa namna hii”, alisema Mwambungu.

Pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa vitendo vya wizi na ubadhirifu wa miradi ya maendeleo unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu katika halmashauri, umesababisha serikali kushindwa kuboresha huduma zake za kijamii kwa wananchi licha ya ukweli kwamba imekuwa ikijitahidi kutafuta fedha na kutenga bajeti yake mwaka hadi mwaka, kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

“Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na manispaa katika mkoa huu nawaagiza  komesheni vitendo vya wizi na tabia ya kuhujumu miradi ya maendeleo, kumekuwa na vitendo vya kihuni katika usimamizi na utekelezaji wa miradi mingi hakikisheni mnawapeleka mahakamani watumishi wote wezi ambao wamekuwa chanzo cha umaskini”, alisisitiza.

Mwambungu amelazimika kutoa kauli hiyo, kufuatia halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini kuwasimamisha kazi watumishi wake wanne ambao ni wakuu wa idara kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma pamoja na kushindwa kusimamia vyema majukumu yao ya kazi.

Wakuu wa idara waliosimamishwa kazi ni mwana sheria wa halmashauri hiyo Hotay Thuway, ofisa ushirika Shekiheri Massawe, ambao wao wana kesi  za jinai katika mahakama ya wilaya Songea, mhandisi wa maji John Undiri na mhandisi wa ujenzi Daud Basilio ambao tuhuma zao ni za kushindwa kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.

Mbali na agizo hilo, Mwambungu  amezitaka halmashauri za wilaya katika mkoa wa Ruvuma kuanza sasa utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia njia za kisasa za mashine za elektroniki (EFDS) ambazo zinasaidia udhibiti wa fedha zinazokusanywa, badala ya kuendelea na utaratibu wa kizamani  wa kutumia risiti za mkono  mfumo ambao umekuwa ukifujisha mapato mengi.

Katika hatua nyingine alisema, halmashauri ya wilaya ya Songea inao uwezo mkubwa wa kuwa ya mfano katika ukusanyaji mapato mkoani humo, hivyo jambo hilo linahitaji kuwa na watumishi wanaojituma, waadilifu, waaminifu na wenye uchungu na halmashauri yao katika kutekeleza kazi zao ipasavyo.

No comments: