Sunday, February 7, 2016

VURUGU ZAKWAMISHA UCHAGUZI CHUO KIKUU SONGEA



Na Mwandishi wetu,

Songea.

UCHAGUZI Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph tawi la Songea mkoani Ruvuma, umeshindwa kufanyika kwa kile kinachodaiwa kuwa uongozi husika wa chuo hicho umekuwa ukiingilia na kutaka kupanga safu ya uongozi wanaoutaka wao, huku wanachuo wakishindwa kuwa huru kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Kufuatia kuwepo kwa hali hiyo, kumesababisha vurugu za hapa na pale katika eneo hilo la chuo, ambazo zilipelekea mmoja wa viongozi wa chuo hicho ambaye ni mtawa aliyefahamika kwa jina moja la Magdalena, raia wa kutoka nchi ya India kunusurika kipigo kutoka kwa wanafunzi wakati alipokuwa akitangaza uchaguzi huo hautafanyika.

Habari zaidi kutoka kwenye chuo hicho zinaeleza kuwa, mapema miezi mitatu iliyopita wanafunzi wa chuo hicho walitangaziwa kuwa mwanachuo yeyote anayetaka uongozi achukue fomu ya kugombea, na hili lilitokana baada ya uongozi uliokuwa madarakani kuisha muda wake wa utawala.

Wanachuo hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, waliwaambia waandishi wa habari kuwa baadaye mchakato wa kuwapata viongozi uliendelea ambapo wagombea walijitokeza na kuanza kufanya kampeni za kuomba wachaguliwe kwa nafasi walizoomba.


Waliongeza kuwa siku chache zilizopita baadhi ya majina ya wagombea yalikatwa na uongozi wa chuo cha Mtakatifu Joseph na kuletwa majina mengine ya wanachuo ambao hawakuomba kugombea, jambo ambalo lilianza kuleta mgogoro na vurugu baina ya wanachuo na uongozi wa chuo ambao unatuhumiwa kuwapangia safu viongozi wanaowataka wao.

Siku ilipowadia ya kufanya uchaguzi Februari tatu mwaka huu, ndipo mtawa Magdalena aliitisha mkutano wa wanachuo wote na kuwatangazia kuwa uchaguzi wa serikali ya wanachuo umefutwa hadi pale watakapotangaziwa tena na kwamba mchakato huo unapaswa kuanza upya, ndipo vurugu hizo zilipoanza kujitokeza.

“Mara baada ya kiongozi huyu kutangaza uchaguzi umefutwa, wanachuo tulishindwa kujizuia, lengo letu tulitaka tupate ufafanuzi juu ya sababu za msingi za kufutwa kwa uchaguzi huu”, walisema wanachuo hao.

Walisema kuwa kutokana na kuwepo kwa migogoro ya mara kwa mara kwenye chuo hicho, baadhi ya wanachuo wameonyesha kusikitishwa kwa mwenendo mzima wa uongozi husika ambao ndio unadaiwa kuwa chanzo cha migogoro na wameiomba serikali kuona umuhimu wa kuingilia kati, ili kuweza kumaliza hali hiyo isiweze kuendelea kujitokeza mara kwa mara.

Pamoja na mambo mengine, wanachuo waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi zilizotangazwa kuwa ni; kwa nafasi ya urais wa serikali ya wanafunzi alikuwa John Zabron na Jonas Kawelela, makamu wa rais George Ngao na Veronica Lusagira.

Kadhalika kwa majina mawili ya wagombea yaliyokatwa na uongozi wa chuo na wanafunzi hao kuanza kuzua tafrani kuwa ni; Jonas Kawelela ambaye inadaiwa jina lake liliondolewa na uongozi huo kwa madai kuwa alifeli somo moja na badala yake nafasi hiyo ilichukuliwa na Silvester Joseph, pia kwa nafasi ya makamu wa rais jina la Veronica Lusagira liliondolewa kwa madai kuwa tangu alipojiunga na chuo hicho miaka miwili iliyopita alikuwa bado hajasajiliwa.

Wanachuo kadhaa walichukuliwa na jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, kwa lengo la kwenda kuwahoji kufuatia kuwepo kwa vurugu hizo ambazo zilitishia uvunjifu wa amani katika eneo la chuo hicho.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji ambaye hakutaja majina ya waliohojiwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanachuo hao baadhi yao walikamatwa, walihojiwa na kuruhusiwa kurudi chuoni kwao ambapo Polisi wamefungua jalada la uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo kiongozi mmoja wa chuo hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Dkt. Katayi alipohojiwa kwa njia ya simu juu ya sakata hilo alieleza kwa kifupi kwamba uchaguzi huo ulisitishwa, kutokana na baadhi ya wagombea kutotimiza vigezo husika na akaishia kukata simu.

No comments: