Monday, February 15, 2016

WATUMISHI WANNE HALMASHAURI SONGEA WATUMBULIWA MAJIPU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WATUMISHI wanne waliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamesimamishwa kazi na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kutokana na utovu wa nidhamu, wakidaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha na kushindwa kusimamia kikamilifu majukumu yao ya kazi za utumishi wa umma.

Imefafanuliwa kuwa waliosimamishwa kazi kuwa ni wa idara ya ujenzi, maji, ushirika pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea, Rajabu Mtiula alisema kuwa baraza lake limefikia maamuzi hayo baada ya kuridhika na taarifa ya kamati ya fedha, uchumi na mipango kwamba watumishi hao, wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao na kuisababishia hasara halmashauri hiyo.

Mtiula aliwataja  watumishi waliosimamishwa kuwa ni mhandisi wa ujenzi Daud Basilio, mhandisi  wa maji John Undili, ofisa ushirika Sheken Masawe pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Hotay Thuway ambapo kila mmoja alikuwa na tuhuma zake za ubadhirifu.


Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa kwa upande wa mhandisi wa ujenzi Daud  Basilio amesimamishwa kazi, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za mradi wa barabara  ya Mbinga mhalule hadi  Mpitimbi, ambapo mhandisi huyo  alidanganya kuwa ameidhinisha malipo ya kiasi cha shilingi milioni 27  kwa ajili ya  umwagaji kifusi.

Alisema kuwa baada ya wakaguzi kwenda katika eneo la mradi, walibaini kazi iliyofanyika hailingani na kiasi cha fedha kilichoombwa na mhandisi huyo, kwa ajili ya malipo ya mkandarasi husika.

Mtiula alifafanua kwamba pia, Daud  alifanya ubadhirifu katika mradi wa ujenzi wa ghala katika kijiji cha  Mgazini, ambalo imeonyesha kuwa ukarabati wa ghala hilo ulifanywa chini ya kiwango na haulingani na kiasi cha pesa zilizolipwa ambapo zaidi ya shilingi milioni 11.1 hazijulikani zilienda wapi.

Akieleza tuhuma zinazomkabili mhandisi wa maji John Undili alisema kuwa mhandisi huyo, alishindwa kusimamia miradi ya maji kikamilifu na kuonyesha kulikuwa na ubadhirifu kwenye utekelezaji wa miradi ya maji  katika kata ya Matimila, Magagula na Mpitimbi A pamoja na Parangu ambapo  miradi hiyo imeshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuwaondolea kero, wananchi  na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma kama ilivyokusudiwa.

Kadhalika Mwenyekiti huyo  alisema ofisa ushirika, Sheken Masawe ana kesi ya jinai katika Mahakama ya wilaya ya Songea, kuhusiana na ubadhirifu anaodaiwa kuufanya katika chama  cha Ushirika cha Namtumbo  na Songea (SONAMCU) na kusababisha migogoro ambayo imepelekea serikali kuwafikisha Mahakamani.

Mwanasheria wa Halmasahuri hiyo, Hotay Thuway amesimamishwa kazi kwa kuwa ana kesi  Mahakamani ya kujaribu kushawishi kutoa rushwa kwa Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Songea, ili aweze kuwasaidia watuhumiwa waliowavamia maafisa maliasili katika kijiji cha Makwaya kwa kuwapiga na kuwanyanganya silaha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sixbert Valentine alisema  mapendekezo ya madiwani kuwasimamisha kazi watumishi hao ni sahihi kwani wamekwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Hata hivyo aliongeza kuwa uamuzi wa kuwasimamisha ni baada ya kamati ya fedha, uchumi na mipango  kujiridhisha kwamba mhandisi wa maji, John Undili  na mhandisi wa ujenzi Daud Basilio, wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi ipasavyo hivyo kuisababishia Halmashauri hiyo hasara.

No comments: