Monday, February 22, 2016

WATAKAO HUJUMU VIFAA VYA KUTENGENEZA MADAWATI TUNDURU KUKIONA CHA MOTO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

IMEELEZWA kuwa watu watakaojaribu kuhujumu malighafi au vifaa vya kutengenezea madawati, kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi shuleni wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Walimu, mafundi na wananchi wameonywa na wametakiwa kuondokana na mawazo hayo, badala yake wanapaswa kujenga ushirikiano kwa umoja wao ili kazi hiyo ya utengenezaji wa madawati iweze kukamilika kwa wakati.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agnes Hokororo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya maendeleo ya wilaya hiyo, huku akisisitiza kuwa utaratibu huo hautachakachuliwa vinginevyo endapo litatokea tatizo ameunda kikosi kazi na kamati inayofuatilia suala hilo ili kila dawati, liweze kukamilika na kukabidhiwa shuleni kwa ajili ya kuanza kutumika.

"Ofisi yangu imejipanga kikamilifu katika usimamizi wa zoezi hili, nimeunda kikosi kazi na kuteua kamati zinazosimamia ili kudhibiti uchakachuaji wowote unaoweza kujitokeza, wakati wa utekelezaji wa jambo hili", alisema Hokororo. 

Hokororo alisema hayo wakati alipokuwa akijibu pia tuhuma, juu ya uwepo wa taarifa kwamba wapo baadhi ya mafundi wanaoshirikiana na watu wasiokuwa waaminifu, kuhujumu juhudi za maendeleo ya utengenezaji wa madawati ya kukali wanafunzi wilayani humo.


Mkuu huyo wa wilaya alisema, hivi sasa wilaya yake inao upungufu wa madawati 8,000 na kwamba kutokana na agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wilaya hiyo imechukua hatua kwa kutengeneza madawati hayo kwa kutumia mbao zilizokamatwa katika oparesheni tokomeza.

Alisema katika kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa na kukamilika kwa  wakati, kamati yake imejipanga na kuweka taratibu madhubuti kuanzia wakati mafundi hao wanapokwenda kuchukua mbao hizo, kwenye yadi ya idara ya maliasili.

Akifafanua maelezo juu ya uwepo wa taarifa kuwa kuna mbao miongoni mwa hizo zimeonekana kutengenezwa  madirisha na milango ya baadhi ya viongozi na kusafirishwa, alisema hakuna ubao hata mmoja uliotengeneza vitu vya kigogo yeyote na kwamba vifaa hivyo vilitengenezwa kwa ajili ya kufungwa katika hostel ya shule ya sekondari Mataka iliyopo wilayani Tunduru.

Alisema kuwa wilaya  yake yenye shule 173 zikiwemo 23 za sekondari na 150 za msingi, zinakabiliwa na upungufu wa madawati 8,000 na kwamba baada ya kukamilika kwa zoezi la utengenezaji wa madawati hayo, imeandaa mikakati ya kuanza kuwachukulia hatua walimu wakuu ambao shule zao zitaonekana kutokuwa na madawati ya kutosha ya kukalia wanafunzi wote.

Pamoja na mambo mengine Mkuu wa wilaya hiyo, Hokororo alikuwa akihojiwa na waandishi wa habari kama ifuatavyo;

Swali

Nini kilibadilisha mfumo wa awali wa kutengeneza dawati lililounganishwa na vyuma na kuruhusu mbao 3 zitengeneze dawati moja?

Jibu

Hali hiyo ilitokana na baadhi ya mbao hizo kutokuwa katika kipimo kinacho fanana.

Swali

Nini kilichosababisha mbadilishe mfumo wa utengenezaji wa madawati hayo kupitia kituo cha ufundi cha Mataka na badala yake, mkaamua kupeleka mbao hizo shuleni kwa kuwakabidhi walimu ndio wasimamie utengenezaji wake?

Jibu

Jambo hili tulilifanya kwa lengo la kuongeza spidi ya kuharakisha na kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati.

Swali 

Je, mnauhakika gani kwamba walimu hao watatekeleza kazi hiyo kwa ubora unaotakiwa?

Jibu

Tunaamini kwamba, walimu hao watatengeneza madawati yenye ubora unaohitajika kwa vile tayari mafundi wanaowatumia katika maeneo yao walikwisha elekezwa na kupeleka sampuli za kazi zao, katika kamati inayohusika na kuridhika nazo kabla ya kuwaruhusu kufanya kazi hii.

Swali

Mmepanga kutumia utaratibu gani wa kupata mbao ambazo zitasaidia kukamilisha idadi ya madawati yaliyobakia?

Jibu

Wilaya yangu imeandaa mikakati mingi ikiwemo ya kufanya doria na kukamata na kutaifisha mbao zote, zinazogundulika kuwa zimepasuliwa bila kufuata taratibu za uvunaji wa mazo ya misitu pamoja na kutolewa kwa vibali kwa shule zenye upungufu wa madawati, ili waweze kupasua mbao hizo chini ya usimamizi wa kamati yangu.

Swali

Mmeandaa utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa madawati hayo hayatumiwi vibaya au kuharibiwa kwa makusudi na mbao zake, kuuzwa kwa mafundi uashi kutengenezea vitu vingine?

Jibu

Tumeandaa taratibu za kuwachukulia hatua kali za kisheria na kuwawajibisha walimu wakuu na viongozi wengine, ambao watabainika kuhujumu kwa makusudi juhudi hizo zinazofanywa na serikali.

Swali

Mmejipangaje kurejesha mbao hizo endapo zitahitajika na Mahakama au wahusika watashinda kesi ambayo kwa sasa inaendelea mahakamani?

Jibu

Kwanza ofisi yangu haina taarifa kuwa kunakesi ambayo inaendelea juu ya mbao hizo, zaidi ya taarifa kuwa kesi iliyopo serikali ilishinda na wahusika walikwisha hukumiwa kutumikia vifungo vya miaka miwili kila mmoja wao.   

Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa mbao 12,000 zilikamatwa kupitia oparesheni tokomeza chini ya aliyekuwa Waziri wa maliasili na utalii wakati huo, Kagasheki zikiwa zimevunwa bila kufuata taratibu na miongozo inayopaswa kufuatwa wakati wa uvunaji wa mazao hayo ya misitu.

Kwa mujibu wa takwimu hizo kati ya mbao hizo, mbao 6,900 zilikuwa na kesi na zaidi ya mbao 5,000 hazikuwa na kesi na tayari zilikwisha chukuliwa na idara ya magereza iliyoshinda tenda ya kutengenezea thamani za maofisini.

No comments: