Tuesday, February 9, 2016

MVUA ILIYOAMBATANA NA UPEPO MKALI YABOMOA NYUMBA ZA WANANCHI TUNDURU WAKOSA MAHALI PA KUISHI



Na Steven Chindiye,
Tunduru.

MVUA iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika vijiji vya Marumba na Morandi, wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma imeezua na kubomoa nyumba 62 za wananchi na kuwaacha wakiwa hawana mahali pa kuishi.

Taarifa za tukio hilo zinafafanua kwamba mvua hiyo ilianza kunyesha majira ya saa 10 za jioni February 6 mwaka huu, ambazo ziliambatana na radi huku upepo mkali ukianza kuezua mapaa ya nyumba hizo.

Walisema kufuatia hali hiyo, watu waliokumbwa na adha hiyo walianza kukimbia huku na huko wakiwa wanapita kuomba msaada wa kujihifadhi kwa majirani na ndugu zao.


Akizungumzia tukio hilo Diwani wa kata Marumba, Msenga Said Msenga alithibitisha uwepo wa tukio hilo na kuongeza kuwa hivi sasa wahanga wote wamepokelewa na kuhifadhiwa na jamaa zao, katika maeneo jirani wakiwa wanasubiri uwezekano wa kufanya ukarabati au kujenga upya nyumba zao baada ya msimu huu  wa mvua kwisha.

Alisema tukio hilo lilikuwa sio la kawaida ukilinganisha na matukio mengine yaliyowahi kutokea katika vijiji hivyo, na kwamba awali yeye kwa kushirikiana na viongozi wa serikali katika kata yake  walitamani kuwapeleka wahanga hao katika majengo ya shule za serikali, ili kuwahifadhi kwa muda lakini waathirika wote walichukuliwa na kuhifadhiwa katika nyumba za majirani na ndugu zao.

Baada ya tukio hilo na kutoa huduma za awali kwa wahanga hao kukamilika, walipeleka taarifa kwa viongozi wa serikali ngazi ya wilaya, kwa ajili ya kuomba msaada zaidi na kwamba tukio hilo ni la pili kwa wananchi wa vijiji hivyo kukumbwa na mkasa wa aina hiyo ambapo, Januari  mwaka mwaka huu zaidi ya nyumba 21 ziliezuliwa na nyingine kubomolewa na mvua hizo.

No comments: