Saturday, February 27, 2016

DEREVA ASOMBWA NA MAJI WAKATI AKIOGA MTONI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

DEREVA mmoja wa kampuni ya Synohdryo, inayojenga barabara kiwango cha lami kutoka Tunduru mjini kwenda tarafa ya Nakapanya wilayani humo mkoa wa Ruvuma, amefariki dunia baada ya kusombwa na maji.

Dereva huyo ambaye hufahamika kwa jina la, Ally Ramadhani (31) mzaliwa wa  mkoa wa Tanga  alikumbwa na mkasa huo Februari 25 mwaka huu, majira ya saa 11.30 jioni wakati akiwa anaoga katika eneo la mto huo.

Taarifa za tukio hilo zinasema kuwa marehemu huyo alienda kuoga katika mto Muhuwesi, baada ya muda wa kazi kwisha na kwamba aliteleza na kutumbukia mtoni hatimaye kusombwa na mkondo mkali wa maji na kumpeleka kusikojulikana.


Mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba baada ya kuanguka na kutumbukia mtoni, marehemu  alisikika akiomba msaada wa kuokolewa lakini kutokana na wenzake walikuwa hawajui kuogelea waliogopa kujitosa majini, ambapo baadaye kutokana na kukosa msaada wa kuokolewa alizama katika maji na hakuonekana tena, jambo ambalo liliwawia vigumu kumuokoa.

Diwani wa kata ya Muhuwesi  Nurdin Mnolela, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba baada ya taarifa hizo kumfikia yeye kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya kijiji, waliitisha mkutano wa dhalura na kukubaliana  kuanzisha msako wa kuutafuta mwili wa marehemu huyo.

Mnolela alifafanua kuwa licha ya kazi hiyo kuwa ngumu, kutokana na wananchi kutokuwa na ujuzi wa kupiga mbizi, zoezi hilo litawachukua muda mrefu kuupata mwili wa marehemu Ramadhani.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amekiri kutokea kwa tukio hilo na tayari amekwisha tuma kikosi cha vijana kutoka katika jeshi hilo, ili kwenda kushirikiana na wananchi hao katika kuutafuta mwili huo.

No comments: