Monday, February 22, 2016

MKUU WA WILAYA YA MBINGA AWATAKA MADIWANI HALMASHAURI YA MJI WA MBINGA KUTEKELEZA MAJUKUMU YA WANANCHI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MADIWANI katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuondoa itikadi zao za vyama vya kisiasa na kutekeleza majukumu ya kufanya kazi kwa umoja wao, ambayo yataleta manufaa kwa wananchi wanaowazunguka katika maeneo yao.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

“Hatuna sababu hivi sasa kuendeleza malumbano ya kisiasa, Madiwani tunapaswa kufanya kazi za wananchi mambo ya vyama wekeni pembeni, kuendelea kulumbana hakutatufikisha mbali”, alisema Ngaga.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Simon Ngaga.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya, akizungumzia suala la maendeleo katika sekta ya elimu aliwataka pia madiwani hao katika mipango yao wafikirie kujenga majengo mapya ya shule za msingi na sekondari, ili waweze kuwa na shule ambazo zitaweza kutosheleza mahitaji ya watoto waliopo sasa.

Ngaga alisema kuwa licha ya Halmashauri ya mji wa Mbinga, kuwa na upungufu wa madarasa ya kusomea wanafunzi, pia inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa madawati ya kukalia watoto hao.


Pamoja na kupongeza jitihada zinazochukuliwa sasa katika kuyatengeneza madawati hayo ili kukabiliana na tatizo hilo, alieleza kuwa hali sio nzuri watoto ni wengi darasani na hulazimika wakati wa vipindi vya masomo kukaa kwa kugeuza mabenchi ya kukalia, kutokana na uwepo wa uhaba wa madawati.

“Upungufu wetu wa madawati ni mkubwa mno, nimetoa agizo kwa maafisa tarafa na kata washirikiane pia katika jambo hili, tuweze kufikia malengo ya kumaliza tatizo hili”, alisema.

Vilevile alitoa agizo kwa watendaji husika wa Halmashauri hiyo, kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la upungufu wa vyoo kwani baadhi ya shule hazina vyoo vya kudumu, jambo ambalo ni kero kwa walimu na wanafunzi.

Kadhalika katika suala la utunzaji wa mazingira Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, Ngaga alisisitiza kwamba kila mwananchi anapaswa kuyalinda katika hali ya usafi na kwamba suala la uchafu kila mmoja wao, alisema anapaswa kulichukia na kupenda usafi.

Awali akizungumza katika kikao hicho cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji huo, naye Mkurugenzi mtendaji Oscar Yapesa alisema kuwa wameendelea kuboresha mji huo kwa kuuweka katika mazingira mazuri na kufanya usafi mara kwa mara katika maeneo mbalimbali.

Yapesa aliongeza kuwa, anawashukuru wadau wa mji wa Mbinga kwa kushiriki kikamilifu katika suala la usafi wa mazingira kwani wamekuwa wakijitolea kutoa vifaa vya kufanyia usafi, michango ya fedha na magari ya kuzolea taka kuzunguka mji huo.

“Kama mnavyoona mji wetu unapendeza, jitihada hizi hatuna budi kuwashukuru wafanyabiashara na wadau mbalimbali ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha jambo hili, Madiwani nasi kwa umoja wetu tunapaswa kushirikiana kwa kuunga mkono suala hili na tuweze kufikia ufanisi mzuri wa malengo tuliyojiwekea ndani ya Halmashauri yetu”, alisema Yapesa.

No comments: