Friday, February 26, 2016

SONGEA NA MADABA WAPONGEZWA KUGAWANA MALI BILA MVUTANO



Na Stephano Mango,
Songea.

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Songea na Madaba mkoani Ruvuma, wamepongezwa kwa kuridhia mgawanyo wa mali kwa pande zote mbili, bila kuwepo na mvutano kama ilivyo kwa baadhi ya halmashauri zingine mkoani humo.

Pongezi hizo zilitolewa na Katibu tawala wa mkoa huo, Hassan Bendeyeko alipokuwa akizungumza  kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Songea na Madaba kilichokuwa kikijumuisha mgawanyo wa mali, rasilimali na madeni kilichofanyika mjini hapa.

Bendeyeko alisema kuwa madiwani wa halmashauri hizo mbili, wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na halmashauri zingine mkoani humo na kuwataka kuendeleza zaidi mahusiano na kuheshimu makubaliano waliyotiliana sahihi, kwenye mkataba wa mgawanyo wa mali hizo.


Aliwahimiza madiwani wa halmashauri hizo kuona umuhimu wa kuongeza vyanzo vya mapato na kuwa wabunifu, katika kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo itakayopunguza kero za wananchi. 

Naye Mwenyekiti wa halmashauri mama ya Songea, Rajabu Mtiula ambaye alikuwa akiendesha baraza hilo la mgawanyo wa mali alisema kuwa hekima na busara, zilizofanywa na halmashauri hizo mbili zimeonyesha ukomavu wa hali ya juu katika kujadili hoja zenye maslahi kwa pande zote mbili.

Kwa upande wake naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Madaba, Vastus Mfikwa aliipongeza kamati maalum ya mgawanyo wa mali iliyokuwa inaongozwa na Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Bendeyeko kwa namna walivyofanikisha kugawana mali hizo kwa usawa bila kuwepo manung’uniko yoyote.

Mapema akisoma waraka wa mgawanyo wa mali kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Katibu tawala wa wilaya ya Songea ambaye alikuwa katibu wa kamati ya mgawanyo wa rasilimali hizo, Juma Ally alisema kuwa mali zitakazogawanywa ni pamoja na mali zinazohamishika yakiwemo magari na mitambo ya kutengenezea barabara na zile zisizohamishika ambazo ni nyumba pamoja na viwanja.

Halmashauri ya wilaya ya Songea toka kuanzishwa kwake imefanikiwa kuzaa halmashauri ya Manispaa ya Songea, wilaya ya Namtumbo na Madaba.

No comments: