Wednesday, March 2, 2016

WATAKIWA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANACHAMA wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo hapa nchini, wametakiwa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kasi anayoendana nayo sasa ya kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unaboreshwa zaidi,  kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Mwenyekiti, Arka Mgina ambaye ni wa chama cha ushirika cha akiba na mikopo,  Mahanje SACCOS kilichopo katika halmashauri ya Madaba  alisema hayo alipokuwa akizungumza  waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano, tangu ilipoanza kufanya kazi imeonyesha wazi kuwa inapingana vikali na watu waliopewa dhamana ya kuongoza taasisi na  mashirika mbalimbali ya umma, ambao wanatabia mbaya ya ubadhirifu wa mali za wananchi.


Mgina aliiomba serikali hiyo kuendelea na msimamo huo, wenye lengo la kuwasaidia watu wake wenye kupenda haki, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Alisema kuwa ipo haja sasa kwa serikali, kusaidia vyama vya akiba na mikopo kwa kutoa ruzuku ili viweze kukabiliana na changamoto iliyopo ya wakulima wa zao la mahindi hapa nchini, kushindwa kuuza mahindi yao kutokana  na kutokuwepo kwa soko la uhakika.

Vilevile alitumia fursa hiyo, kuwahimiza wanawake kutumia nafasi ya kujiunga na vyama hivyo vya ushirika ambavyo mwisho wa siku vitaweza kuwasaidia na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo alisema Mahanje SACCOS, kimeweza kujenga mahusiano mazuri na taasisi za kifedha kama vile benki na kufanikiwa kuwa na jengo ambalo linatumika katika shughuli mbalimbali za chama na tayari kimenunua kiwanja kingine kwa ajili ya kujenga ofisi mpya ya kisasa, pamoja na ghala la kuhifadhia nafaka pamoja na kusomesha watoto yatima ambao wamefiwa na wazazi wao waliokuwa wanachama wa chama hicho cha akiba na mikopo.

No comments: