Saturday, March 26, 2016

WAKULIMA WA KAHAWA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA KASI YA USAMBAZAJI WA MADAWA

Ofisa ugani wa Taasisi ya kituo cha utafiti zao la kahawa TaCRI, Daniel Mwakalinga ambaye yupo kati kati amevaa shati lenye rangi nyeupe akitoa elimu ya kilimo bora cha zao la kahawa kwa wakulima wa kijiji cha Mkinga kata ya Mapera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma ambapo wakulima hao aliwataka kutumia miche ya kahawa aina ya vikonyo ambayo haishambuliwi na wadudu waharibifu.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wanaolima zao la kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali ya awamu ya tano hapa nchini, kuongeza kasi ya usambazaji wa madawa yanayodhibiti zao hilo lisishambuliwe na wadudu waharibifu, ili waweze kuzalisha kahawa kwa wingi na yenye ubora.

Aidha walieleza kuwa ugonjwa wa Chulebuni (CBD) ni ugonjwa ambao huenea kwa kasi, ambapo mti wa kahawa ulioshambuliwa na ugonjwa huo hupoteza asilimia 90 ya mavuno endapo mkulima hatazingatia namna ya kuzuia ugonjwa huo.

Rai hiyo ilitolewa na wakulima hao kwenye maadhimisho ya siku ya mkulima wa kahawa yaliyofanyika kijiji cha Mkinga kata ya Mapera wilayani hapa, ambapo Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa TaCRI wilayani humo imejiwekea utaratibu wake kila mwaka wa maadhimisho hayo, ikilenga kuelimisha wakulima juu ya kilimo bora cha zao la kahawa.


Siku hiyo ya mkulima wa kahawa, kumekuwa na utaratibu wa kukutana pamoja na wenzao na kubadilishana uzoefu wa uzalishaji wa zao hilo, kwa viwango vinavyokubalika katika soko la kimataifa.

Wakulima hao walieleza kuwa ugonjwa wa CBD huathiri matunda ya kahawa, ambapo hushambulia mbuni wa kahawa hasa nyakati za masika pale maua yanapochanua, punje zinapokuwa changa na zinapoelekea kuiva hivyo serikali haina budi kuongeza kasi ya usambazaji wa pembejeo za kilimo cha zao hilo kwa wakati.

Christian Mapunda ambaye ni mkulima wa kijiji cha Mkinga, akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake alisema kuwa wakulima wa zao hilo ili waweze kuepukana na usumbufu huo wa kahawa zao mashambani kushambuliwa na wadudu waharibifu, ni vyema serikali ikaendelea na utaratibu wa kutoa ruzuku kwenye miche bora ya kahawa aina ya vikonyo ambayo huzalishwa na TaCRI na kusambazwa kwa wakulima.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Ofisa kilimo na mifugo wa wilaya ya Mbinga, Yohanes Nyoni aliwataka wakulima hao kuzingatia kanuni za kilimo bora cha zao hilo kwa kushirikiana na maofisa kilimo waliopo katika maeneo yao.

Nyoni alisema kuwa, wakulima hao wanapaswa pia kutumia mitambo ya kisasa pale wanapokoboa kahawa mbivu mara baada ya kuichuma shambani, ili iweze kuwa na ubora unaokubalika.

Vilevile Ofisa kilimo huyo alikemea biashara haramu ya magoma, ambapo wafanyabiashara wajanja hupita kwa wakulima vijijini na kuwarubuni wawauzie kahawa mbivu, kwa bei ndogo ikiwa bado shambani haijavunwa na kumfanya mkulima mwisho wa siku aendelee kubaki kuwa maskini.

“Tushirikiane kuwadhibiti wafanyabiashara hawa, soko la kahawa linahitaji kuimarisha ushirikiano lazima tujiunge kwenye vikundi au vyama vya ushirika, tuache kufanya biashara ya kahawa mtu mmoja mmoja”, alisisitiza Nyoni.

No comments: