Tuesday, March 22, 2016

AKAMATWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUKUTWA NA BUNDUKI KINYUME NA TARATIBU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI wa kijiji  cha Namiungo  wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Abdul Pushapusha (56) anashikiliwa na Polisi, kwa tuhuma za kukutwa na bunduki kinyume na taratibu za umiliki wa silaha za moto.

Aidha katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na risasi moja ya bunduki aina ya Rifle na maganda matano ya risasi za bunduki aina ya Shortgun kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema.


Akifafanua taarifa hiyo, Kamanda Mwombeji alisema kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa alifanyiwa upekuzi na kukutwa akiwa na bunduki hiyo inayodaiwa kwamba, ilikuwa ikitumika katika matukio ya kiuhalifu.

Alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa, alikuwa akiitumia kwa mtindo wa kuikodisha kwa watu ambao walikuwa wakifanya matukio ya uwindaji haramu wa tembo, katika mapori ya hifadhi wilayani Tunduru na pori la Niasa lililopo nchi jirani ya Msumbiji.

Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo, kwa ajili kujibu shtaka lililopo mbele yake ili sheria iweze kuchukua mkondo wake baada ya taratibu husika kukamilika.

No comments: