Saturday, March 26, 2016

SOUWASA YALIA NA WAHARIBIFU WA MAZINGIRA YASEMA ATAKAYEKAMATWA KUFIKISHWA MAHAKAMANI



Na Julius Konala,
Songea.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepiga marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji, ikiwa ni lengo la kukabiliana na tatizo la ukame linaloweza kujitokeza kipindi cha kiangazi.

Aidha imeelezwa kuwa kwa mwananchi atakayebainika kukiuka agizo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Mhandisi uzalishaji wa mamlaka hiyo, Jones Salema alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo, Mhandisi Francis Kapongo.


Salema alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa, baada ya kubaini kwamba baadhi ya wananchi hufanya uharibifu mkubwa wa kuchoma moto na uchafuzi wa mazingira kwenye chanzo cha Lipasi, kilichopo katika milima ya Matogoro kitendo ambacho huisababishia mamlaka hiyo hasara kubwa na hulazimika kununua madawa ya kutibu maji hayo.

“Pamoja na kupiga marufuku wananchi kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji, bado baadhi ya wananchi wenye kiburi wamekuwa wakikaidi na hata kuendesha shughuli za kilimo katika vyanzo hivyo, tunasema tutakayemkamata atachukuliwa hatua za kisheria”, alisema.

Naye Mhandisi Emmanuel Kinunda wa mamlaka hiyo, alisema kuwa kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika chanzo cha Lipasi kilichopo kwenye milima ya Matogoro, inapaswa kuwekewa ulinzi mkali kwa kuunda vikundi mbalimbali vya kusimamia vyanzo hivyo.

Kinunda amewaomba wananchi wa Manispaa ya Songea, kushirikiana na Mamlaka katika kukabiliana na hali hiyo kwa madai kuwa kuna baadhi ya wananchi, bado wanaendelea kuendesha shughuli za kibinadamu pia kwenye chanzo cha mto Luhira, ambacho nacho ni tegemeo kubwa la utoaji wa huduma ya maji kwa  wakazi wa Manispaa hiyo.

Kwa upande wake Meneja msaidizi Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Songea, Juma Mbwambo alisema kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo la msitu wa milima ya Matogoro kuchomwa moto, ofisi yake imejipanga katika kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo yote ya vyanzo vya maji pamoja na kutengeneza njia za kukabiliana na hali hiyo.

No comments: