Tuesday, March 8, 2016

WANAFUNZI NAMABENGO WASIMAMISHWA MASOMO KUTOKANA NA KUKOSA NIDHAMU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANAFUNZI 10 kati ya 106 wanaosoma kidato cha sita, shule ya sekondari Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamesimamishwa kuendelea na masomo katika shule hiyo kwa muda wa wiki tatu, kutokana na kukosa nidhamu na kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Maandamano hayo walifanya wakielekea kwa Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu kwa lengo la kupeleka malalamiko yao dhidi ya Makamu mkuu wa shule hiyo, Shaibu Champunga wakimtuhumu kuwa na lugha na tabia chafu na vitisho kwa wanafunzi hao.

Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo, Alkwin Ndimbo alipozungumza na mwandishi wetu alisema kwamba baada ya wanafunzi hao kufanya maandamano hayo, zilifanyika jitihada za kuwarudisha shuleni kwa lengo la kubaini chanzo cha maandamano hayo huku akimwagiza Ofisa elimu wa sekondari wilayani humo, Patrick Atanas ahakikishe anachukua hatua za haraka kwa kukutana na viongozi wa shule na wanafunzi hao, ili kuona tuhuma zinazomkabili Makamu mkuu wa shule hiyo.


Ndimbo alieleza kuwa, baada ya Ofisa elimu Atanas na uongozi wa shule na wanafunzi wote kukaa pamoja na kuangalia chanzo cha tatizo hilo ilibainika kuwa wanafunzi 106 kutoka Namabengo hadi kijiji cha Mlete, umbali wa kilometa 16 walifanya kosa la kuandamana bila kufuata taratibu husika.

Walisema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu na wamevunja kanuni na sheria za shule hiyo kwa kuondoka eneo la shule bila idhini husika, ambapo kwa kufanya kosa hilo wanafunzi hao walikiri na uongozi wa shule uliamuru wanafunzi 96 wachapwe viboko vitatu kila mmoja, huku 10 ambao ndio walikuwa vinara wa maandamano hayo wamesimamishwa masomo kwa muda wa wiki tatu na mara watakapomaliza adhabu hiyo watatakiwa waende na wazazi wao, kwa hatua zaidi za kinidhamu.

Alisema kuwa tuhuma ambazo wanafunzi hao walimtuhumu mwalimu Champunga, sio za kweli kwani katika mahojiano mbalimbali yaliyofanyika hakuna aliyeweza kuthibitisha tuhuma hizo, hivyo hawawezi kumchukulia hatua bila kuwa na ushahidi wa kutosha.

Malalamiko ya watoto hao yalifuatia ikidaiwa kwamba, Champunga amekuwa akiwatolea vitisho na lugha za matusi kwa wanafunzi, kuwachapa viboko visivyo na idadi, amekuwa akiingia kwenye bweni la wanafunzi wa kike nyakati za usiku bila kufuata taratibu na kulazimisha kufanya nao mapenzi akimtoa nje ya bweni mwanafunzi wa kike anayemtaka.

Kutokana na malalamiko hayo walitaka kwenda kumwona Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mwambungu ili aweze kuwasikiliza na kupatia ufumbuzi wa kero zao na kwamba juhudi za kutaka kuonana na Mkuu huyo wa mkoa, ziligonga mwamba baada ya kuzuiwa na askari Polisi wa wilaya ya Namtumbo.

Wanafunzi hao walizuiwa wakiwa kijiji cha Mlete, wakielekea kwa Mkuu huyo wa mkoa ambapo kijiji hicho kipo nje kidogo ya Manispaa ya Songea ambapo askari Polisi walipoingilia kati, waliamuru wasimame na kuwataka waeleze sababu ya kufanya maandamano bila kibali, ambapo wanafunzi hao walieleza kuwa kila mtu ana haki ya kuongea kwa kuwa walishatoa malalamiko yao kwa Mkuu wao wa shule lakini hawajasikilizwa, hivyo waliona ni vyema malalamiko yao wakayafikishe kwa Mkuu wa mkoa huo.

Muda mfupi baada ya kuwasili Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo, Alkwin Ndimbo na kusikiliza malalamiko ya wanafunzi hao dhidi ya  Makamu mkuu wa shule ya sekondari Namabengo, Shaibu Champunga kwamba hawamtaki shuleni hapo kwa sababu ya vitendo hivyo vichafu anavyowafanyia.

Pamoja na mambo mengine, walilalamikia pia shule hiyo haina miundombinu mizuri ambapo walidai kuwa vyoo vilivyopo ni vibovu havifai kutumika, baadhi ya madarasa hayana sakafu na kwamba wanalazimika kwenda umbali mrefu kufuata huduma ya maji.

Baada ya viongozi hao kusikiliza malalamiko ya wanafunzi hao, waliwataka warudi shuleni ili wakatoe maamuzi mbele ya wanafunzi wote pamoja na walimu wao jambo ambalo, wanafunzi walilikubali na kusitisha maandamano hayo.

No comments: