Sunday, March 6, 2016

WANAWAKE RUVUMA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA NAFASI ZA UPENDELEO

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, Farida Mdaula wa tatu kushoto akifurahia jambo na baadhi ya wanawake wenzake Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, baada ya kufungua zoezi la uoshaji magari kwa ajili ya kupata fedha za kusaidia watoto wenye mahitaji muhimu na wale wanaoishi katika mazingira magumu, wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa kamapuni ya MM Intertaiment iliyoratibu zoezi hilo, Maretha Msembele.


Na Muhidin Amri,
Songea.

KUELEKEA siku ya wananawake duniani ambayo kila mwaka inafanyika Marchi 8, serikali imeombwa kuongeza nafasi za upendeleo kwa wanawake ili  kuwaongezea uwezo  wa kiutendaji, hasa pale wanapoteuliwa kushika  nafasi mbalimbali za uongozi na kuwaongezea nguvu katika kukabiliana na  changamoto zinazowakabili mbele yao katika maisha yao ya kila siku.

Rai hiyo ilitolewa jana mjini Songea na Mwanaharakati wa masuala ya wanawake na mfanyabiashara maarufu, anayeuza mafuta ya kuendeshea mitambo mbalimbali mkoani Ruvuma,  Farida Mdaula wakati  alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanawake wa Manispaa ya Songea, ambao waliamua kushiriki katika zoezi la usafi wa kuosha magari kwa ajili ya kutafuta fedha za kusaidia  watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale waliokacha kwenda shule kwa kukosa mahitaji muhimu.

Alisema wanawake wengi wanakabiliwa na umaskini, hasa wa kipato na kukosa fursa ya kushirikishwa kwenye vyombo vya maamuzi na hata katika umilikaji wa rasilimali, licha ya ukweli kwamba ndiyo kundi  kubwa linalochangia maendeleo na kukua kwa uchumi wa nchi yetu.


Kwa mujibu wa Mdaula alisema kwamba, wanawake wakipewa nafasi katika vyombo hivyo kama vile Makahama, Bunge au nafasi za kuteuliwa ikiwemo ukuu wa wilaya, mkoa na hata kuwa wakurugenzi wa halmashauri itasaidia kuwa na uwezo katika kukabiliana na hali ya umaskini kwa  kuwa, wale  watakaopata nafasi hizo watajitokeza  kuwapa elimu na maarifa  wanawake  wenzao.

“Sikatai kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, wakati wa utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete wanawake wamepata nafasi nyingi za uongozi katika nchi hii, hata hivyo sisi kama wanawake tunahitaji nafasi hizo  ziongezwe zaidi ili tuweze kuwa sawa na wanaume”, alisema Mdaula.

Vilevile aliwataka wanawake kuushinda moyo wao, kwa kujiepusha kufanya vitendo ambavyo vinawavunjia heshima mbele ya jamii badala yake  wafanye kazi halali  za kujipatia kipato, ikiwemo kazi ya kuosha magari ambayo kwa sasa  ina faida kubwa  kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya magari.

Mbali na hilo, Mdaula amewashauri wanawake wa mkoa huo na kote nchini kujitokeza kukopa fedha katika taasisi za fedha kama vile mabenki, vyama vya kuweka na kukopa ili waweze kuanzisha miradi ya kiuchumi, itakayoweza kuwafanya waendeshe maisha yao na sio muda mwingi kuishi kwa kuwategemea waume zao.

“Wanawake ni muhimu sana, waache tabia ya kizamani ya utegemezi kwa wanaume, kwani licha ya kuwa mume ndiyo mwenye wajibu wa kutafuta riziki ya kila siku kwa ajili ya familia, hata hivyo na sisi tusikae na kusuburi kutoka kwao kwani tutaendelea  kukabiliwa  na umaskini  katika maisha yetu”, alisema.

Katika hatua nyingine Mdaula, amewaonya wanawake kuacha tabia ya kupigana  majungu na hali ya kukatishana tamaa wakati huu ambao bado kundi hilo linakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, ikilinganishwa na wanaume hivyo ni muhimu wapeane moyo na kufarijiana hasa pale mmoja wao anapopata matatizo.

Pamoja na mambo mengine, Mdaula ambaye pia ni kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa mkoani Ruvuma, amewakumbusha wanawake wenzake kuwa mstari wa mbele kupeleka watoto wao shule badala ya kuwafanyisha kazi za nyumbani, ambazo  kwa muda mrefu zimekwamisha ndoto za vijana wengi kuendelea na maisha yao katika kupiga mbele hatua mbalimbali.

No comments: