Saturday, March 5, 2016

MWAMBUNGU RUVUMA AWATAKA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA UADILIFU

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu, watatu kutoka upande wa kulia akiwa na viongozi wengine wa mkoa huo wakiongoza kikao cha RCC.



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

SAID Mwambungu ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, amewataka watumishi wa umma katika mkoa huo watekeleze majukumu yao ya kazi za kila siku kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu mkubwa ili wananchi wanaowatumikia waweze kunufaika na matunda ya serikali yao.

Alisema kuwa endapo watazingatia hilo, wataweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima na kuleta ufanisi sehemu ya kazi na kwamba, huduma watakazotoa kwa jamii zitakuwa bora zaidi.

Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, alitoa rai hiyo jana alipokuwa akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa.

Kwa mujibu wa Mwambungu alieleza kwamba, maadili mema katika kazi za utumishi wa umma ndio silaha kubwa hivyo kila mtumishi akizingatia hilo wataweza pia kuepukana na tabia mbaya, ya kuomba na kupokea rushwa ambavyo ndio adui mkubwa katika ustawi wa maendeleo ya wananchi.


“Serikali ya awamu ya tano tunazingatia ukweli na uimarishaji wa utawala bora ndiyo njia sahihi ya uhakika katika kuondokana na matatizo kama vile ya ufisadi, umaskini na utoaji wa huduma mbovu kwenye taasisi za umma, katika mkoa huu tuepukane na mambo yanayokwamisha maendeleo yetu katika jamii”, alisema Mwambungu.

Vilevile alipozungumzia suala la huduma za  afya, Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa serikali itaendelea kuboresha na wananchi wataweza kupata huduma bora katika vituo vyake vya afya, zahanati na hospitali mbalimbali. 

Alisema kuwa katika kukabiliana na tatizo la msongamano wa wagonjwa katika maeneo hayo ya kutolea huduma za afya, serikali mkoani Ruvuma inaendelea na mkakati wa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuitaka halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo na Manispaa ya Songea kukamilisha haraka ujenzi wa hospitali zake za wilaya, pamoja na kuimarisha vituo vya afya vilivyopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo.

Mbali na hilo, Mwambungu amezitaka pia halmashauri zote katika mkoa huo kuendelea kuimarisha vituo hivyo kwa kila kata, ili watu wengi wahudumiwe huko badala ya kukimbilia hospitali ya rufaa mjini Songea, ikiwemo sambamba na viongozi kuweka mikakati ya kukamilisha ujenzi wa majengo ya kutolea huduma.

Akizungumzia juu ya tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta hiyo, alisema ni changamoto ambayo serikali inaifahamu na inalifanyia kazi ikiwemo kuongeza vifaa tiba pamoja na dawa.

Pia Mwambungu amewaagiza wakurugenzi kuendelea kutekeleza agizo la serikali la kusimamia na kukusanya fedha, kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (EFDS) kwa kile alichofafanua kwamba mfumo huo utasaidia kupunguza upotevu wa mapato ya serikali.

No comments: