Wednesday, March 9, 2016

DIWANI HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA AFARIKI DUNIA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

DIWANI wa kata ya Maguu wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Nathaniel Hyera kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amefariki dunia, kutokana na kupata tatizo la ugonjwa wa shinikizo la damu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Ambrose Nchimbi alisema kuwa Hyera alifikwa na mauti Marchi 8 mwaka huu, majira ya asubuhi wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo.

Nchimbi alisema kuwa halmashauri yake, inasikitika kumpoteza diwani huyo kwani alikuwa ni mtu ambaye anatoa ushauri mzuri na kupigania maendeleo ya wananchi wake na wilaya hiyo kwa ujumla.


“Marehemu alikuwa ni mjumbe wa kamati ya fedha, mipango na uongozi alikuwa akitushauri kwa karibu katika kupanga mipango mbalimbali ya kimaendeleo, kwa kweli tunasikitika kumpoteza kiongozi huyu wa wananchi”, alisema Nchimbi.

Alifafanua kuwa mwili wa marehemu huyo umesafirishwa kwenda kijijini kwao Maguu, ambako mazishi yatafanyika leo Marchi 10 mwaka huu majira ya saa 8:00 mchana.

Pamoja na mambo mengine alifafanua kuwa madiwani, viongozi na wananchi kwa ujumla wilayani Mbinga wamekwisha julishwa kwenda kuhudhuria mazishi hayo, na kwamba aliwaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

No comments: