Tuesday, March 15, 2016

WANAFUNZI NALWALE TUNDURU WASHTAKI WAZAZI WAO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANAFUNZI shule ya msingi Nalwale, iliyopo katika kata ya Nandembo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamewashtaki wazazi wao kwa uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwamba, wamekuwa wakipuuzia utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na mfuko huo.

Wanafunzi hao walibainisha hayo, wakati walipotembelewa na viongozi kutoka TASAF ngazi ya mkoa na wilaya na kuwashuhudia watoto hao, wakisoma wakiwa hawana sare na viatu miguuni mwao.

Aidha walifafanua kwamba mbali na wao kutambua umuhimu wa kuwapatia huduma hizo, bado wamekuwa wakipuuza na badala yake hutumia fedha zinazotolewa na mfuko  kwa shughuli nyingine.

Mwanafunzi Abibi Said anayesoma darasa la tatu katika shule hiyo, alisema kuwa kila anapomweleza baba yake amnunulie sare na viatu ili na yeye apendeze kama wenzake, amekuwa akijibiwa kuwa fedha alizopokea kupitia utaratibu wa uhaulishaji fedha kwa kaya maskini amezitumia kununulia mbolea.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mratibu wa TASAF mkoa wa Ruvuma, John Nginga na mshauri wa mfuko wilaya ya Tunduru, Christian Amani waliwaonya wazazi na walezi wote wanaotumia fedha hizo kinyume na maelekezo yanayotolewa na mfuko, kwamba watafungiwa kuendelea kuzipokea.

Kufuatia hali hiyo viongozi hao wakamwagiza Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nalwale, Abdi Mkwate na Ofisa mtendaji wa kijiji Swalehe Hassu kuwafuatilia na kuwabaini wazazi na walezi wote ambao hawajatimiza masharti ya kuwanunulia watoto wao sare za shule, katika malipo yatakayofuata waondolewe.

Awali akitoa taarifa kwa viongozi hao, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nalwale Grace Ngonyani alisema jumla ya watoto 132 kati ya wanafunzi 301 ya wanafunzi wote wanaosoma shuleni hapo, wananufaika kupitia mpango huo.

Katika taarifa hiyo, Ngonyani aliipongeza serikali kwa kubuni na kuanzisha mpango huo ambao alisema kwamba, umesaidia kupunguza utoro na kuongeza ufaulu katika shule yake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Abdi Mkwate na mtendaji wake, Swalehe Hassu waliwahakikishia viongozi hao kwamba watatekeleza maelekezo hayo kwa wakati ili kuwezesha watoto hao, kuendelea na masomo.

No comments: