Tuesday, March 8, 2016

AUAWA KWENYE CHUMBA CHA MAHABUSU NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

ERASTO Nditi (31) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kindimba juu wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Nditi aliuawa akiwa kwenye chumba cha mahabusu, katika Ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho baada ya kuvamiwa na wananchi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Marchi 3 mwaka huu majira ya saa 2:30 usiku.

Mwombeji alifafanua kuwa, wananchi hao walichukua maamuzi hayo magumu wakidai kwamba marehemu huyo enzi ya uhai wake alikuwa mkorofi, mwizi na amewahi kumkata mwananchi mwenzake, upanga mkononi wakati alipokamatwa akiiba.


Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa, kufuatia tukio hilo wamekamatwa watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, ambapo wanaendelea kuhojiwa na kwamba uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo.

Pamoja na mambo mengine, Kamanda Mwombeji alitoa mwito kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake wanapowakamata watuhumiwa wawafikishe kwenye vyombo vya sheria.

Katika tukio jingine, Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Sophia Mussa (62) amekutwa shambani akiwa amefariki dunia huku mwili wake ukiwa na majeraha sehemu ya kichwani, yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Mama huyo ni mkazi wa kijiji cha Nakapanya kata ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, na kwamba mwili wake ulikutwa huko shambani Marchi 3 mwaka huu majira ya mchana.

Kufuatia tukio hilo anashikiliwa kijana mmoja mkazi wa kijiji hicho (jina limehifadhiwa) ambaye Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa huo, ameeleza kuwa alikuwa pamoja na mama huyo wakilima na baadaye alikimbia baada ya kudaiwa kufanya kitendo hicho cha mauaji.

No comments: