Tuesday, March 22, 2016

AKUTWA BARABARANI AMEFARIKI DUNIA AKIWA AMEPONDEKA KICHWA NA MBAVU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Mabatini, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma Omary Rashid (64) amekutwa akiwa amefariki dunia, katika tukio la kugongwa na gari au pikipiki.

Zubery Mwombeji.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema waliuona mwili wa marehemu huyo ukiwa umelala barabarani eneo la mabatini jambo ambalo liliwafanya wahisi kwamba, huenda marehemu aligongwa na vyombo hivyo vya moto.

Mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Abdala Issa, alisema kuwa huenda chanzo cha kifo chake kilisababishwa na tabia yake ya ulevi wa kupindukia na kwamba, baada ya kuzidiwa na pombe alilala barabarani na hivyo kugongwa bila kujitambua.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na wanaendelea kufanya uchunguzi, ili kuweza kujua chanzo cha kifo chake.


Aidha alisema wamejipangga kufanya uchunguzi wa kina kwa lengo la kuhakikisha kwamba, mtuhumiwa aliyefanya kosa hilo anakamatwa na sheria kuchukua mkondo wake.

Kufuatia hali ya utata uliopo juu ya tukio hilo, Kamanda Mwombeji alisema Polisi wanawaomba wananchi wenye taarifa za tukio hilo kutoa ushirikiano wa karibu, ili waweze kumkamata mhusika kwa urahisi zaidi.

Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Rashid, Dkt. Gaufrid Mvile alisema kuwa kifo hicho kilisababishwa na kutokwa na damu nyingi, baada ya ajali hiyo kutokea.

Dkt. Mvile alifafanua kuwa, marehemu alivunjika mguu wa kushoto na kuvurugika mbavu za pande zote mwilini mwake, pamoja na kupasuka fuvu la kichwa chake.

No comments: