Tuesday, March 15, 2016

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUSHAMBULIWA NA FISI WAKATI AMELALA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Jiungeni kata ya Mchesi, tarafa ya Lukumbule  wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mohamed Kilapile (75) amefariki dunia baada  ya kushambuliwa na fisi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo zinaeleza kuwa, fisi huyo alimvamia Kipalile na kumkata kichwa huku akiachanisha kiwiliwili chake na kutoweka nacho, kwa ajili ya kwenda kula nyama yake.

Tukio hilo lilitokea Marchi 9 mwaka huu, majira ya usiku wakati marehemu huyo akiwa amelala katika nyumba yake, ambayo haikuwa na mlango.

Godfrey Manyahi ambaye ni Afisa tarafa ya Lukumbule, alithibitisha kuwepo kwa mauaji hayo na kwamba hilo ni tukio la pili kutokea katika tarafa hiyo, mwaka huu.


Alisema tukio la kwanza lilitokea Februari 29 mwaka huu, kijiji cha Imani kwenye mashamba yaliyopo kandokando mwa hifadhi ya msitu wa Mwambesi katika tarafa hiyo ambapo pia, fisi aliripotiwa kumuua na kumkata kichwa mkazi mmoja wa kijiji cha Lukumbule Mwanabibi Yusufu (70) ambaye sasa ni marehemu.

Akifafanua juu ya kifo cha Kilapile, Afisa tarafa huyo alisema kuwa siku ya tukio hilo marehemu alikuwa amelala peke yake ndani ya nyumba hiyo aliyokuwa akiishi na kwamba, mnyama huyo mkali alikuwa amemvamia na kumshika kichwani wakati akiwa amelala usingizi.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo mwili wake, ulikutwa ukiwa na majeraha sehemu za mikononi, miguu, makalio pamoja na paja la mguu wa kulia.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dkt. Zabron Mmari alisema chanzo cha kifo chake kilisababishwa na kitendo cha kukatwa kichwa chake, kulikosababisha kutokwa na damu nyingi.

Naye Afisa ardhi na maliasili wilayani humo, Japhet Mnyagala alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba tayari amekwisha tuma askari wake ambao wana silaha kwa ajili ya kwenda kumsaka na kumuua fisi huyo, ili asiendelee kuleta madhara kwa watu wengine.

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba, Polisi bado wanaendelea na uchunguzi ili kuweza kupata ukweli zaidi juu ya kifo hicho.

No comments: