Wednesday, March 9, 2016

WALIMU MBINGA WALALAMIKIA MAOFISA KUWATOLEA LUGHA MBAYA

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamewalalamikia baadhi ya maofisa wa halmashauri ya wilaya hiyo kuwatolea lugha mbaya pale walimu hao, wanapokwenda katika ofisi za maofisa hao kupeleka shida zao za kikazi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Aidha wamesikitishwa na utunzaji mbaya wa kumbukumbu zao, jambo ambalo linasababisha walimu hulazimika kurudia kuzipeleka zaidi ya mara moja hasa pale wanapodai malimbikizo ya mishahara yao, na kwamba katika ofisi zinazohusika na kushughulikia tatizo hilo kuna baadhi ya walimu hawajafanyiwa hesabu za malimbikizo yao kwa muda mrefu.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Mbinga, Wernery Mhagama alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya chama hicho wilayani humo, katika uzinduzi wa mafunzo ya siku moja ya walimu Wawakilishi mahali pa kazi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Taarifa hiyo, ilikuwa ikitolewa kwa Ofisa utumishi wa wilaya ya Mbinga, Mwajuma Kihiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo.


“Kwa muda mrefu baadhi ya walimu wangu hawajapandishwa vyeo kwa wakati na hasa pale inapotokea wale walioajiriwa pamoja, kupishana mwaka wa kupanda vyeo chama kinaendelea kuwatambua hao na wewe ukiwa mwajiri uone namna ya kuwakutanisha katika cheo kimoja, ukitaka unaweza……….”, alisema Mhagama.

Vilevile Katibu huyo wa CWT aliwataka watumishi wanaowahudumia walimu wilayani humo, wajitambue kuwa kila mmoja ni zao lililotokana na mwalimu hivyo wana kila sababu ya kuwasikiliza na kuwatimizia kwa wakati mahitaji yao ya msingi, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima mahali pa kazi.

Pamoja na mambo mengine, wilaya ya Mbinga mafunzo hayo yanaendeshwa katika vituo saba na kwamba washiriki 280 watanufaika na kukifahamu chama chao na kwenda kufikisha manufaa hayo, kwa wanachama wenzao wanao wawakilisha.

Mafunzo hayo yalihusisha mada zinazowafanya waweze kutambua; dhima ya chama cha wafanyakazi, chama cha walimu Tanzania na katiba yake, wajibu wa mwakilishi mahali pa kazi, utatuzi wa migogoro kazini, sheria mbalimbali zinazohusu walimu, muundo wa utumishi wa walimu na usimamizi wa fedha na utunzaji wa mali za chama.

Awali akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Ofisa utumishi wa wilaya hiyo Mwajuma alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kusema kuwa tayari wamekwisha anza kuzifanyia kazi, hivyo walimu wanapaswa kujenga ushirikiano na kuacha kulalamika mitaani badala yake waende katika ofisi za idara ya utumishi wilayani humo, ili aweze kutatuliwa matatizo yao.

Akijibu hoja juu ya walimu kutopandishwa vyeo kwa wakati na kutofanyiwa hesabu za malimbikizo ya mishahara yao kwa muda mrefu, Ofisa utumishi huyo alieleza kuwa matatizo hayo yanasababishwa na kitengo cha Mamlaka ya Nidhamu ya Walimu (TSD) wilayani humo.

Mwajuma alieleza kuwa kitengo hicho cha TSD wamekuwa hawapeleki taarifa zilizokamilika katika idara yake ya utumishi kwa wakati, hivyo alishauri walimu watunze kumbukumbu zao vizuri na kuziwasilisha wenyewe katika ofisi hiyo, ili kumaliza matatizo yaliyopo mbele yao.

“TSD tunagombana nao hapa wilayani kila siku, utakuta tunaletewa taarifa za mtu anayestahili kupandishwa cheo huku zikiwa tofauti hazijakamilika, tunaendelea kubanana nao watuletee taarifa nzuri za mtumishi ambazo zimekamilika ili tuweze kuzifanyia kazi vizuri”, alisema Mwajuma.


No comments: