Thursday, March 24, 2016

BMT YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUFICHUA MATATIZO YALIYOPO KWENYE KLABU ZA MICHEZO


Na  Kassian Nyandindi,

Songea.

MJUMBE wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hapa nchini, Zainabu Mbiro (Pichani) amewaomba waandishi wa habari wasaidie kufichua migogoro iliyopo katika klabu za michezo ili mamlaka husika, ziweze kuchukua hatua na kuweza kuondokana na matatizo yaliyopo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo katika sekta ya michezo.

Mbiro alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa mkoani Ruvuma, ambapo pia aliipongeza timu ya Majimaji mkoani humo kwa kuendelea vizuri katika michezo mbalimbali ya soka.


Kadhalika alitoa rai kwa kamati za mpira wa pete mkoani humo, kuhakikisha kwamba wanakwenda hadi katika ngazi za wilaya kuunda kamati ambazo zitaweza kuimarisha mchezo wa netiboli, na kuwa endelevu.

Alisema kuwa vyama vya michezo hapa nchini, viongozi wake wasipokaa na kuviendesha vizuri, hawataweza kuvifanya visonge mbele na kuifanya jamii ishindwe kufikia malengo yake katika sekta ya michezo.

“Waandishi wa habari narudia tena kutoa wito kwenu, mtusaidie kufichua matatizo yanayosababisha sekta hii ya michezo ishindwe kusonga mbele, fichueni ili wahusika waweze kuwajibika ipasavyo”, alisema.

Mbiro ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Netiboli Tanzania (CHANETA) na pia Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya alisisitiza kuwa viongozi husika waliopo madarakani katika vyama vya michezo, kuzingatia maadili ya kazi zao ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima miongoni mwa wadau wa michezo hapa nchini.

No comments: