Saturday, March 5, 2016

MKOA WA RUVUMA UNA ZIADA YA TANI MILIONI 1 ZA MAHINDI

Wakuu wa wilaya za mkoa wa Ruvuma, wakipokea maagizo ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na namna wanavyopaswa kusimamia utekelezaji huo.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKOA wa Ruvuma una  ziada ya chakula tani milioni 1 za mahindi, ambazo zimetokana na ongezeko la uzalishaji katika msimu wa kilimo wa mwaka 2014/2015  uliofikia tani milioni 1.564,283 huku mahitaji halisi ya wananchi wake waishio katika mkoa huo, ni tani 469,172.

Uzalishaji wa zao hilo katika msimu huo, mkoa ulifanikiwa kuzalisha tani 689,123 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17.3.

Kwa  mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika kipindi cha mwaka jana, zinaonesha kuwa wastani wa pato la mtu mmoja (Per capital income ) mkoani humo, limezidi kukua kutoka shilingi milioni 1,913,526 kwa mwaka 2013/2014 hadi kufikia shilingi milioni 2,082,167 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 8 kwa mwaka 2014/2015.


Hayo yalisemwa  na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo  (RCC) kilichofanyika mjini hapa, na kuhimiza wananchi kutobweteka  na mafanikio hayo badala yake waongeze juhudi katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Mwambungu alisema, kwa takwimu hizo zinaonesha mkoa huo ni wa tano kitaifa ukitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro na Arusha hata hivyo alifafanua kuwa malengo waliyojiwekea ndani ya mkoa huo ni kushika nafasi ya kwanza, ifikapo mwaka 2018 katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Alieleza kuwa mkoa unaendelea  kupiga hatua nzuri katika ukuaji wa uchumi unaoendana na kuboresha maisha ya wananchi wake, ambapo serikali nayo inaendelea kuwahudumia wananchi hao kwa kutoa huduma bora hasa kwenye nyanja ya elimu, afya, maji pamoja na suala zima la utawala bora.

Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, aliongeza kuwa changamoto kubwa iliyopo sasa ni matumizi  hafifu ya zana bora za kilimo kwa wakulima wake, kama vile Matrekta makubwa ya kulimia kwani hadi kufikia Disemba mwaka jana mkoa huo ulikuwa na Matrekta 171 kati yake 103 ni yale yaliyonunuliwa mwaka 2012 kutoka Suma JKT, ambapo lengo ni kufikia Matrekta 200 ifikapo  msimu ujao wa kilimo.

Kadhalika alitoa mwito kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi katika halmashauri za mkoa huo, kusimamia kikamilifu na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaohujumu sekta ya kilimo huku akiagiza usimamizi wake uende kwa kasi hadi katika ngazi ya kijiji, na kwamba serikali itaendelea kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya kuuzia mazao yao.

No comments: