Monday, March 14, 2016

MBINGA YABAINI KAYA ZISIZOSTAHILI MPANGO WA TASAF

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga hivi karibuni akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake wilayani humo ikiwemo akiwataka wananchi kujiunga na vikundi vya ujasiariamali.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

OFISI ya Mkurugenzi mtendaji, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imefanya ufuatiliaji na kubaini kwamba, baadhi ya wanufaika waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya hiyo hawana vigezo vya kuendelea kupata ruzuku katika mpango huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo, Ahasante Luambano alisema kuwa ofisi yake itaendelea kufanya ufuatiliaji mara kwa mara ili kuweza kuzibaini kaya hizo kwa utekelezaji zaidi.


Luambano alifafanua kuwa kaya tano ambazo majina yao yamehifadhiwa, zimeondolewa katika mpango ambapo watu hao wanaishi katika kijiji cha Mbinga na kwamba wameondolewa kabisa, kutokana na majina yao hayakustahili kupewa ruzuku.

Mratibu huyo wa TASAF aliongeza kuwa, makubaliano ya kuwandoa yalifanyika katika kikao maalum kilichoketi kwenye uwanja wa shule ya msingi Kiwanjani iliyopo mjini hapa, ambacho kiliwakutanisha walengwa wote waliopo kwenye mpango katika kijiji hicho na hatimaye kufikia maamuzi hayo.

“Tumeyaondoa majina ya watu watano, kutokana na kutokuwa na vigezo vya kuendelea kuwa kwenye mpango wa kunusuru kaya hizi maskini hapa wilayani, natoa mwito kwa wananchi waendelee kujenga ushirikiano kwa kutupatia taarifa sahihi katika maeneo mengine, ambayo wanaona kuna matatizo kama haya”, alisema Luambano.

No comments: