Monday, March 21, 2016

WANANCHI KILOSA JUU WAMLALAMIKIA MKUU WA WILAYA YA NYASA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.


BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Kilosa juu, wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma wamemlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo, Margaret Malenga kwa kutumia amri ya kuwataka wahame katika maeneo yao wanayoishi kabla ya kulipwa fidia zao, ili waweze kumpisha mwekezaji anayetaka kutumia sehemu ya eneo la kijiji hicho kujenga kituo cha kuuza mafuta.

Aidha walisema kuwa wameshangazwa na kitendo hicho, wakidai kuwa anatumia nguvu kutaka wananchi hao waondoke jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi, hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati ili waweze kupata haki yao ya msingi.

Walisema kuwa wasipopewa malipo ya fidia zao ipasavyo, kamwe hawataweza kuhama mpaka utakapofanyika upembuzi yakinifu, juu ya malipo hayo katika maeneo yao wanayoishi.

Kadhalika walieleza kuwa, kumekuwa na usiri mkubwa uliogubikwa juu ya mwekezaji huyo ambapo mnamo Marchi 9 mwaka huu ulifanyika mkutano kijijini hapo na Mkuu huyo wa wilaya, na pale walipomtaka aeleze bayana juu ya nani anayetaka kuwekeza katika eneo hilo hakutaka kumtaja.


“Huyu Mkuu wa wilaya sisi anatushangaza sana, wakati tulipofanya mkutano wa kijiji wananchi waliuliza maswali ya kumtaka hili jambo lisiwe linafanyika kwa usiri, watu walipohoji na kumtaka atuambie ni nani anayetaka kuja kujenga kituo hiki cha kuuzia mafuta, alikataa kuwaeleza wananchi”, alisema Said Hussein mkazi wa kijiji hicho.

Naye Ester Mahepano aliongeza kuwa watu walipokuwa wakihoji kutaka kujua ukweli na uwazi juu ya jambo hilo, Mkuu wa wilaya ya Nyasa Malenga alikuwa akiwajia juu na kuonesha ukali kama mbogo huku akitumia amri ya kuwataka wakae chini wale waliokuwa wakihoji.

Vilevile walisema kuwa baada ya wiki moja kupita, walimwona Mkuu huyo wa wilaya akiwa katika maeneo yao na wataalamu wa idara ya ardhi toka Halmashauri ya wilaya ya Nyasa wakianza kupima maeneo yao, bila kuwashirikisha wananchi kitendo ambacho
walisema anatumia vibaya madaraka yake hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati na kuweka sawa jambo hilo, ili kuweza kunusuru madhara yanayoweza kutokea hapo baadaye.

“Huyu Mkuu wa wilaya tumemwona akiwa na watu wa ardhi wakizunguka katika maeneo yetu wakipima ardhi, toka ameanza mchakato huu hajatushirikisha wananchi ipasavyo haya mambo anayafanya peke yake akiwa na viongozi wenzake wa halmashauri”, alisema Yakobo Komba.

Diwani wa kata ya Kilosa Stanley Vumu alipohojiwa juu ya malalamiko hayo ya wananchi alikiri kuwepo akidai kuwa tayari hatua husika zimeanza kuchukuliwa kwa lengo la kumaliza mgogoro huo, ambao unaweza kukwamisha shughuli mbalimbali za kijamii.

“Hili zoezi la kupima yale maeneo tumesitisha kwanza, tutaendelea na mchakato siku zijazo baada ya wananchi watakapokuwa wameelimishwa na kuelewa juu ya umuhimu wa kujenga kituo hiki cha mafuta, katika wilaya yetu”, alisema Vumu.

Vumu aliongeza kuwa ni vyema serikali kupitia watendaji wake wakaliweka sawa suala hilo, ili wananchi waweze kupata haki zao na kwamba aliwataka wananchi wake kuwa watulivu wakati yeye akiwa diwani wao akiendelea na jitihada za kuwasiliana na mamlaka husika.

Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Jabir Shekimweri alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo alisema wao wanatarajia kupima eneo lenye ukubwa wa ekari moja na nusu, huku nyumba nane katika eneo hilo wanatarajia kuzibomoa baada ya kulipwa fidia wananchi wenye nyumba hizo.

Shekimweri alifafanua kuwa wawekezaji wanaotarajiwa kujenga kisima cha mafuta katika eneo hilo lenye mgogoro ni watatu ambapo kati yao aliwataja wawili ambao ni kampuni ya Camel na Oil com huku akikataa kutaja kampuni ya tatu.

Mkuu wa wilaya hiyo, Malenga alisema eneo hilo katika mchoro wake limetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa aina mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kulielewa hilo na kwamba yeye kama Mkuu wa wilaya ataendelea kulisimamia hilo.

Hata hivyo aliwaasa wananchi wenye maeneo hayo, kupeleka malalamiko yao ofisini kwake pale itakapoonekana wamepunjwa malipo yao ya fidia na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kulipatia suala hilo umuhimu wa kipekee jambo ambalo litapelekea kumaliza mgogoro huo.



No comments: