Saturday, March 5, 2016

JENERALI MILANZI AWATAKA WANARUVUMA KUTUNZA VIVUTIO VYA UTALII

Mnara wa Mashujaa wa watu waliokufa, wakati wa vita vya Majimaji hapa mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKOA wa Ruvuma, umetakiwa kuona umuhimu wa kuendelea kutunza vivutio vya utalii na kutumia fursa ya uwepo wa vivutio hivyo, kama njia mojawapo ya kujipatia kipato badala ya kuwaachia watu wengine kutoka nje ya mkoa huo wanufaike na rasilimali zilizopo ndani ya mkoa.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani humo, kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya Mashujaa wa vita vya Majimaji na utalii wa utamaduni, yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa vilivyopo Mahenge mjini hapa.

Jenerali Milanzi alisema kuwa serikali kupitia shirika la makumbusho ya Taifa, ipo tayari kutoa utaalamu na miongozo kwa wadau wote ambao wapo tayari kuanzisha makumbusho katika maeneo ya ndani na nje ya mkoa huo, ili kuweza kutoa fursa mbalimbali za uwepo wa vivutio vingi hapa nchini.


Alifafanua kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi kuona umuhimu wa kuibua, kuanzisha na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na matumizi endelevu ya urithi wa utamaduni wetu, kwa lengo la kujipatia ajira na kuchangia kupunguza umaskini wa kipato katika jamii.

Pamoja na mambo mengine, Jenerali Milanzi amezishauri halmashauri za wilaya, manispaa, majiji, taasisi za watu wa umma na watu wengine binafsi kujenga utamaduni wa kutunza kumbukumbu pamoja na kuanzisha makumbusho na kuviweka katika hali nzuri ya kuwa vituo vya mafunzo na vivutio vya utalii.

Alibainisha kuwa sera na sheria zinazosimamia urithi wa tamaduni zetu hapa nchini, zinaruhusu sekta binafsi kuwekeza katika shughuli hizo ambapo jukumu la serikali ni kutoa miongozo na taratibu za matumizi endelevu ya urithi wa tamaduni hizo.

Vilevile aliipongeza serikali ya mkoa wa Ruvuma, chini ya usimamizi wa Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu, kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza uendelezaji wa utalii na urithi wa tamaduni zake.

Hata hivyo aliongeza kuwa hatua na juhudi zinazofanywa na serikali ya mkoa huo zinapaswa kuigwa na viongozi wa mikoa mingine hapa nchini, ili vivutio vya utalii na urithi wa utamaduni viweze kuchangia katika kutoa ajira, kuongeza kipato na kupunguza umaskini katika jamii.


 

No comments: