Sunday, March 6, 2016

MM INTERTAINMENT KUSAIDIA WATOTO YATIMA SONGEA

Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Ruvuma, Sikudhani Chikambo upande wa kulia, akikabidhi fedha taslimu shilingi laki moja jana kwa Mratibu na Mkurugenzi wa MM Intertainment, Marietha Msembele kama mchango wake kwa ajili ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Songea. 

BAADHI ya wanawake katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametumia siku ya mwisho wa wiki kufanya zoezi la kuosha magari katika mitaa mbalimbali ya Manispaa hiyo mjini hapa, ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
 
Mkurugenzi wa kampuni ya MM Intertainment iliyopo mjini hapa, Marietha Msembele ambaye ndiye Mratibu wa zoezi hilo  alisema kuwa wameamua kufanya hivyo, kwa kuuweka mpango huo kuwa endelevu na utalenga  kukusanya shilingi milioni  10 ambazo zitapelekwa kusaidia kununulia vifaa vya shule kama vile sare, viatu, vitabu, daftari na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya watoto hao ambao wapo katika Manispaa hiyo.

Alisema kuwa licha ya serikali, kutangaza na kuanza kutekeleza suala la elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne nchini kote, hata hivyo bado kuna watoto ambao hadi sasa hawajaripoti katika shule hizo kutokana na kukosa mahitaji  muhimu na wapo bado majumbani, hivyo yeye na kampuni yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameamua kufanya hivyo ili kuweza kusaidia watoto hao.


Alifafanua kuwa kuna idadi kubwa ya watoto bado wapo mitaani wanazurula kutokana na kukosa mahitaji hayo muhimu, ambao wameshindwa kuanza  masomo yao  au kukatisha masomo yao.

Msembele aliongeza kwamba kuna watoto wengine wameshindwa kuanza kidato cha kwanza, kwenye shule za sekondari walizopangiwa wakihofia kupata aibu kwenda shule kutokana na kukosa sare au viatu.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu mkoani Ruvuma, Sikudhani Chikambo ambaye alizindua zoezi hilo katika viwanja vya Chama cha Mapinduzi mkoani hapa,  aliwapongeza wanawake hao kwa uamuzi wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu na wale walioshindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa mahitaji hayo muhimu.

Alisema mkakati huo endapo utasimamiwa vizuri, utasaidia kuongeza idadi ya watoto mashuleni kwa kile alichoeleza kuwa tayari serikali ya awamu ya tano imeshaanza utekelezaji wa ahadi zake, kutoa elimu bure kwa watoto wote hapa nchini.

Chikambo aliziomba taasisi, makampuni na watu binafsi kuwaunga mkono wanawake hao ambao kutokana na  kuguswa na matatizo yanayowakabili Watanzania wenzao, wameamua kutafuta fedha  kwa kuosha magari bila kujali urembo na uzuri walionao.

Pia alieleza kuwa wanawake ni watu muhimu katika kukuza uchumi wa taifa lolote lile hapa duniani, hivyo nguvu yao inakosa mashiko kwa sababu wanawake wenyewe wamekuwa ni kundi linalokubali  kuridhika na kipato kidogo inachopata, huku  wengine wakiamua kutafuta fedha kwa njia haramu ikiwemo kuuza miili yao.

Hata hivyo amewaasa wanawake wa mkoa wa Ruvuma, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya kuwaingizia mapato, ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

No comments: