Thursday, March 3, 2016

NALICHO AWATAKA WAKULIMA NAMTUMBO KUENDELEA NA KILIMO CHA ZAO LA TUMBAKU

Zao la Tumbaku.

Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

CHANDE Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo  kuacha mara moja  kuwakumbatia viongozi wa vyama vya  ushirika wanaotajwa kuhusika na wizi wa fedha za wakulima, kwani  endapo watafanya hivyo watasababisha wakulima hao washindwe kusonga mbele kimaendeleo na kubakia kuwa maskini.

Nalicho  ametoa kauli hiyo hivi karibuni, alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti  na wananchi wa kata ya  Lusewa wakati akikagua shughuli za kilimo na  zoezi la uandikishaji wa  wanafunzi   wenye sifa ya kuanza elimu ya awali, msingi na wale walioteuliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu.

Aidha amewataka wananchi na wanachama wa vyama hivyo, kuwafichua viongozi wa vyama vya ushirika ambao wanahusika hasa katika wizi wa pembejeo za kilimo na  mali za chama, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Alisema kuwa madiwani ni wawakilishi wa wananchi, hawapaswi kuwafumbia macho na kuwalinda viongozi wezi, kwani vitendo hivyo vinasababisha wakulima kuwa maskini na kushindwa kuendesha maisha yao.


“Madiwani  ni wawakilishi wa wananchi, lazima watambue wajibu wao wa kuwasaidia wananchi, yatupasa kuwatendea haki na sio kukaa kimya pale tunapoona wanadhulumiwa mali zao”, alisema.

Vilevile alisikitishwa na ukimya wa baadhi ya madiwani hao na viongozi wengine ngazi ya kijiji na kata, kushindwa kukemea wizi unaofanyika kwenye vyama hivyo vya ushirika.

Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo alieleza kuwa atahakikisha anazunguka kwa wananchi katika kila kata wilayani humo, ili kuweza kubaini viongozi wa vyama vya ushirika wanaotajwa kuhusika na vitendo hivyo vya  wizi.

Nalicho amemtaka  kila diwani katika kata yake, kutoa taarifa  ya maendeleo ya wananchi  ikiwemo  mwenendo wa vyama  vya ushirika ambako kuna matatizo ya ubadhirifu wa fedha za wanachama.

Katika hatua nyingine, amewasihi wakulima wa wilaya hiyo kuendelea na kilimo cha zao la tumbaku licha ya ukweli kwamba, bado wakulima hao kwa kiasi kikubwa wanakabiliwa na matatizo mengi katika kilimo cha zao hilo.

Alibainisha kuwa tayari serikali imeshaanza kuyashughulikia matatizo yao na kwamba hawapaswi kukata tamaa, kwa kuwa zao hilo ndilo zao pekee   la kibiashara  wilayani Namtumbo licha ya wilaya hiyo, kuzalisha mazao mengine kama vile ufuta na mbaazi.

No comments: