Tuesday, March 8, 2016

WATIWA MBARONI KWA KOSA LA KULIMA BANGI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma, linawashikilia wakazi wawili wa kijiji cha Mseto na Liparamba wilayani Nyasa mkoani humo kwa tuhuma ya kukutwa wakiwa wamelima  mashamba mawili ya bangi,  yenye ukubwa wa ekari tano  ambayo inadaiwa kwamba yamekuwa yakitegemewa na watu wanaojihusisha na  biashara haramu ya kuuza bangi wilayani humo.

Zuberi Mwombeji.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Thadei Ngonyani (26) mkazi wa kijiji cha Mseto na Philimoni Kumburu (58) wa Liparamba ambapo wote walikamatwa juzi majira ya saa za mchana.

Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na oparesheni yake kabambe katika maeneo mbalimbali mkoani humo, dhidi ya watu hao wanaojihusisha na kilimo cha zao la bangi na  kwamba msako huo ulianza  katika wilaya ya Nyasa.

Kamanda Mwombeji alieleza kuwa katika tukio la kwanza huko katika kijiji cha Mseto kilichopo kata ya Liparamba, tarafa ya Mpepo askari Polisi wakiwa kwenye msako huo walifanikiwa kumkamata Ngonyani, akiwa amelima zao hilo katika shamba lenye ukubwa wa ekari tatu.


Alieleza kuwa katika shamba hilo, Ngonyani alikuwa amechanganya na mazao mengine pembeni yakizunguka shamba hilo, kwa lengo la kuficha bangi ambayo ilikuwa katikati ya shamba isiweze kuonekana.

Katika tukio la pili  inadaiwa kuwa Kumburu ambaye ni mkazi wa kijiji cha Liparamba naye alidakwa na askari hao, baada ya kubainika anashamba la bangi lenye ukubwa wa ekari mbili ambalo ndani ya shamba hilo ameotesha miche mingi ya bangi huku pembeni akiwa amepanda mahindi, kwa lengo la kuficha nayo isiweze kuonekana kwa urahisi.

Aliongeza kuwa mara tu baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, taratibu za kuharibu bangi hiyo zilifuata, sambamba na kuiteketeza kwa moto chini ya ulinzi mkali wa Polisi na kwamba watuhumiwa watafikishwa Mahakamani mara tu upelelezi utakapokamilika.

Katika tukio kama hilo, naye Khaji Kipande (29) mkazi wa mtaa wa Songea boys Manispaa ya Songea na Alphonce Tamaldini (25) wa kata ya Majengo wilayani Tunduru mkoani hapa, walikamatwa na askari Polisi wakiwa na kete za bangi.

Kipande alikamatwa na kete 83 alizokuwa amezihifadhi kwenye mfuko wa rambo nyeusi katika kibanda chake cha biashara, huku Tamaldini alikamatwa na kete 70 akiwa nazo kwenye nyumba ya kulala wageni mtaa wa Mtanda wilayani humo ambapo watafikishwa Mahakamani, kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments: