Monday, March 21, 2016

WAFUNGWA TUNDURU WAFARIKI DUNIA BAADA YA KUPIGWA RADI GEREZANI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAFUNGWA wawili ambao walikuwa wakitumikia kifungo katika gereza la kilimo na mifugo Majimaji, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi.

Sambamba na vifo hivyo, pia watatu walijeruhiwa baada ya kupigwa na radi hiyo na kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya matibabu zaidi ambako wamelazwa na hali zao bado ni mbaya.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya jioni Marchi 18 mwaka huu, wakati wafungwa hao wakiwa wamekwisha fungiwa gerezani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ni mipango ya Mungu, hivyo hakuna wa kumlaumu.


Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni mfungwa namba 15/2016 Hassan Mtewa (32) mkazi wa kijjiji cha Nandembo wilayani humo, ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia katika kosa la wizi wa kuku.

Kamanda Mwombeji alimtaja mwingine aliyefariki kuwa ni mfungwa namba 29/2015 Issa Daudi (40) mzaliwa wa wilaya ya Namtumbo mkoani hapa, ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia katika kosa la kuvunja na kuiba mifugo.

Pia aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni, Shida Haulle mzaliwa wilaya ya Mbinga ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia katika kosa la wizi.

Wengine ni Mhamudu Msusa mkazi wa Nandembo wilayani Tunduru ambaye  alikuwa anatumikia kifungo cha mwaka mmoja, sawa na marehemu Mtewa kwa kosa la kuiba kuku.

Kamanda Mwombeji pia alimtaja majeruhi mwingine, aliyekumbwa na mkasa huo kuwa ni Akandu Abdallah mkazi wa kijiji cha Mchoteka wilayani Tunduru ambaye alikuwa anakabiliwa na adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia katika kosa la kujifanya usalama wa Taifa.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya serikali wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Dkt. Mmari Zabron alithibitisha kuwapokea marehemu hao wawili na majeruhi watatu, Marchi 18 mwaka huu majira ya saa 1 usiku.

Alisema baada ya kuwapokea miili ya marehemu hao, ilihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika hospitali hiyo.

Kuhusiana na hali za majeruhi hao, alisema kuwa juhudi za kuokoa maisha yao zinaendelea na kwamba hali zao kwa sasa zilikuwa zinaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.

Mganga aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu hao, Dkt. Gaofrid Mvile alisema kuwa vifo hivyo vilisababisshwa na mshituko wa shoti ya umeme uliosababishwa na radi hiyo.

Taarifa ambazo zilithibitishwa kutoka kwa baadhi ya askari wa gereza hilo, ambao walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa Jeshi hilo, zinaonesha kuwa ni tukio la nne kwa radi kupiga katika gereza hilo.

Walisema mwaka 2014 radi ilipiga mti mkubwa uliokuwa jirani na gereza lao, mwaka 2015 ilipiga na kuua ng'ombe mmoja na mwaka huu imepiga tena na kusababisha matatizo hayo yaliyotokea jambo ambalo linawafanya waishi kwa hofu.

Kufuatia hali hiyo askari hao wameiomba serikali, kuangalia uwezekano wa kuwafungia vifaa vinavyoweza kusaidia kudhibiti radi hizo, ili zisiendelee kusababisha maafa katika makambi yao na gereza kwa ujumla.

No comments: