Saturday, March 5, 2016

AJINYONGA HADI KUFA HUKU AKIWA AMEACHA UJUMBE MEZANI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKAZI mmoja wa kitongoji cha Halale kilichopo katika kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Francis Nkondora (38) amekutwa akiwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa unaning’inia juu ya mti mrefu, baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani huku mke wake akiwa amemwachia ujumbe mzito nyumbani kwake mezani.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Yahaya Athumani zimesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10 jioni karibu na eneo la mnara wa kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, katika kitongoji hicho.
Zuberi Mwombeji.

Alisema kwamba siku ya tukio hilo, Nkondora na familia yake walikuwa wamepanga kwenda shambani majira ya asubuhi lakini aliwaamuru watoto wake pamoja na mkewe, watangulie kwanza shambani yeye angefuata baadaye.

Alifafanua kuwa familia yake pamoja na mkewe walipotangulia kwenda huko walikaa muda mrefu hawakumwona, na kwamba muda ulipofika wa kurudi nyumbani Nkondora hakuweza kuonekana lakini walipofika nyumbani walikuta barua mezani ambayo ilikuwa imeandikwa na marehemu huyo, kabla hajachukua maamuzi hayo ya kujiua.


Ujumbe uliokuwa umeachwa na marehemu huyo ulikuwa ukieleza kwamba; “Mke wangu urudi nyumbani nisomeshee watoto wangu, nimeamua kujiua mtanikuta kwenye mnara wa simu mkachukue pesa shilingi laki tano kwa mama Deni ili zisaidie watoto hawa, nimechoka kuzurura kudai pesa zangu”.

Kaimu Kamanda huyo wa Polisi alifafanua kuwa watoto wake walipoona ujumbe huo walikwenda hadi kwenye eneo la mnara wa simu, ambako walimkuta baba yao akiwa ananing’inia kwenye mti baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani aliyokuwa ameifunga kwenye mti huo.

“Tulichobaini hapa ni kwamba, marehemu alichukua maamuzi haya magumu baada ya watu anaowadai pesa kumzungusha kwa muda mrefu bila mafanikio, jambo ambalo lilimfanya apate hasira na kujichukulia sheria mkononi”, alisema Athumani.

Kaimu Kamanda wa Polisi Athumani, aliongeza kuwa baadaye watoto wake walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali  ya kijiji cha Kigonsera ambapo walipokwenda kwenye eneo la tukio walishuhudia Nkondora akiwa amejinyonga, baadaye waliwasiliana na uongozi wa Kituo kikuu cha Polisi Mbinga mjini na askari walikwenda huko kwenye eneo la tukio, na kubaini hali hiyo.

Hata hivyo, alieleza kuwa Polisi bado wanaendelea kufanya upelelezi wa kina ikiwa pamoja na kujiridhisha, kama kuna mtu yeyote anayehusika katika tukio hilo ambalo limewaachia majonzi watoto, ndugu jamaa na familia yake kwa ujumla.

No comments: