Saturday, March 12, 2016

WALALAMIKIA KITENGO CHA TAALUMA ELIMU MSINGI SONGEA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KITENGO cha taaluma idara ya elimu msingi, Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kimetupiwa lawama kwa kile kinachodaiwa uwepo wa baadhi ya maofisa elimu wa idara hiyo kuigawa ofisi na kutengeneza makundi, hali ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu katika manispaa hiyo na kuifanya kuwa ya mwisho, katika halmashauri nane zilizopo mkoani humo.

Baadhi  ya walimu, wakuu wa shule za msingi na waratibu elimu kata ambao wameomba majina yao yasitajwe gazetini wameulalamikia uongozi husika kwa kuendekeza chuki na majungu ambayo sasa yanasababisha kuvunjika moyo utendaji kazi kwa baadhi ya watumishi na halmashauri hiyo kuwa ya mwisho kimkoa matokeo ya mtihani wa taifa darasa la saba mwaka jana.

Walisema kuwa ni jambo la aibu kutokea, kwani Manispaa ya Songea ina shule chache ambazo wanaweza kuwafanya wanafunzi wafaulu mitihani yao vizuri kutokana na miundombinu ya shule hizo, kuwa mizuri tofauti na maeneo mengine ndani ya mkoa huo.

Walisema kitendo kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa idara hiyo kinakwamisha maendeleo ya elimu, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuingilia kati na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ili lisiweze kuleta madhara baadaye katika jamii.


“Kutokana na uroho wa madaraka walionao watu wachache katika idara hii ya taaluma na ambao hawana uchungu na taifa hili, kazi yao kubwa ni kukaa na kutengeneza makundi yanayosababisha uzembe kazini na kushuka kwa elimu”, walisema.

Walieleza kuwa hali hiyo endapo itaendelea kuwepo, kuna baadhi ya waratibu elimu kata na walimu wakuu wamejipanga kukwamisha jitihada za kupanda kwa kiwango cha elimu katika manispaa hiyo, kutokana na mgogoro unaoendelea kufukuta kwenye idara za elimu huku wanasiasa nao wakionekana kuendekeza mgogoro huo kwa maslahi yao binafsi.

Waliongeza kuwa makundi hayo yamekuwa yakiyumbisha utendaji kazi wa walimu na kushindwa kutekeleza  majukumu yao ipasavyo, ikiwemo kufundisha watoto darasani.

Kufuatia mkutano maalumu uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya wasichana Songea, kati ya Mbunge wa jimbo la Songea mjini  Leonidas Gama na walimu wa shule za msingi katika manispaa hiyo pamoja na maofisa wa idara ya elimu msingi, walimu hao walimweleza Mbunge huyo changamoto mbalimbali zilizosababisha kuwa wa mwisho katika mtihani wa taifa kimkoa, ikiwemo kuwepo kwa madai ya walimu ya muda mrefu ambayo hayajafanyiwa kazi na idara hiyo kutosikiliza shida na kero mbalimbali zinazowakabili walimu.

Aidha walizitaja changamoto nyingine zilizopelekea kushindwa kufanya vizuri katika mtihani huo, kuwa ni pamoja na walimu kuhamishwa hovyo kwa sababu ya chuki inayotokana na makundi hayo pamoja na uwepo wa matabaka, baina ya baadhi ya maofisa elimu na walimu.

Walisema jipu ambalo lipo kwenye idara ya taaluma, inabidi liondolewe ikiwemo wahusika wanaosababisha hali hiyo kuhamishwa kwenda nje ya mkoa huo ili kuweza kuondoa tofauti zilizopo sasa, ambazo zinasababisha kushuka kwa kiwango cha taaluma na migogoro baina ya waratibu elimu kata na wakuu wa shule za msingi.

Sababu nyingine inayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu  walisema idara kushindwa kugharamia huduma za matibabu pindi mwalimu anapougua, uchache wa walimu pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika darasa moja.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama, alisema kuwa atahakikisha anashirikiana na serikali katika kuangalia uwezekano wa kutatua kero na changamoto zinazowakabili walimu mashuleni, ili waweze kupandisha kiwango cha ufaulu ikiwa pamoja na kupiga marufuku madiwani wenye tabia ya kushinikiza kuhamishwa kwa walimu kusikokuwa na kikomo kwa sababu zao binafsi.

Ofisa elimu msingi Manispaa ya Songea Edith Kagomba, alipohojiwa na mwandishi wetu alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na walimu kuhamishwa mara kwa mara katika vituo vyao vya kazi.

Kagomba alisema kuwa uhamisho huo wa walimu ulikuwa ukishinikizwa na baadhi ya madiwani wa baraza lililopita, kwa sababu ya chuki zao binafsi.

Vilevile Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Jenifa Omolo alisema kuwa analifahamu jambo hilo na tayari, hatua za kiutumishi zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya madai husika.

Pamoja na mambo mengine alipotakiwa kuelezea kwa nini jambo hili limekuwa kero na kusababisha mifarakano katika idara hiyo na kuzalisha watoto wasio na taaluma, Omolo alisema yeye ni mgeni na kwamba atafuatilia kwa karibu ili aweze kulimaliza kwa muda muafaka na hali hiyo, isiweze kuendelea kuwagawa walimu wake.

No comments: