 |
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete, akiwa pamoja na Katibu mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
HATIMAYE Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, leo
imetengua maamuzi ya kurudia kufanya uchaguzi wa kura za maoni katika kata ya
Kihangimahuka na Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia vurugu
zilizoendelea kushika kasi Ofisi za CCM wilayani humo kwa masaa kadhaa, ikidaiwa
kwamba kurudiwa kwa uchaguzi huo kunalenga kumbeba mgombea mmojawapo ambaye alishindwa
katika uchaguzi wa kura hizo zilizofanyika, Agosti Mosi mwaka huu.
Aidha maamuzi hayo yalifikiwa leo jioni hii, baada ya Kamati
ya siasa ya wilaya hiyo kuketi kwa muda wa masaa matano wakijadili suala hilo ikiongozwa na Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho kufuatia wanachama wa chama hicho baada ya kuandamana kuelekea kwenye Ofisi za
Chama wilaya, kupinga kurudiwa kwa uchaguzi huo kwenye kata hizo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda
alisema hayo mbele ya wanachama wa chama hicho ambao walikusanyika kwenye
viwanja vya chama hicho, kusubiri hatma ya majibu hayo yaliyotolewa na Kamati
kuu ya Chama Cha Mapinduzi.
“Ndungu zangu wananchi wa Mbinga, kwa mujibu wa maamuzi
yaliyotolewa na kamati kuu ya chama baada ya kuketi na kujadili suala hili,
wamekubaliana kwamba hakuna uchaguzi utakaoendelea kufanyika, hivyo endeleeni
na shangwe na vifijo msilete fujo”, alisema Mbunda.