Friday, November 27, 2015

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGANA NA LORI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JOVIN Ndunguru (40) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lukanzauti kata ya Mapera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, amefariki dunia papo hapo baada ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha kugongana uso kwa uso na lori ambalo lilikuwa katika mwendo kasi.

Mihayo Msikhela.
Taarifa za tukio hilo zinaelezwa kuwa dereva, Kanisius Ndunguru (32) mkazi wa Mbinga mjini, aliyekuwa akiendesha lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 242 DBL aligongana na pikipiki hiyo, yenye namba T 432 CAN aina ya Fekon akiwa kwenye kona kali kijijini humo ambayo ilikuwa ikiendeshwa na marehemu huyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 25 mwaka huu majira ya saa 8:00 mchana katika kijiji cha Kihulila kata ya Kilimani, barabara ya kuelekea Mbamba bay mjini hapa.  


Alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga, ukisubiri ndugu kwa ajili ya kuusafirisha kwenda kijijini kwao kwa mazishi.

Kadhalika Msikhela aliongeza kuwa dereva wa lori hilo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hilo.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya hiyo, Robert Elisha naye alisema kuwa marehemu alipoteza maisha kutokana na kuvuja damu nyingi, kufuatia majeraha aliyoyapata sehemu mbalimbali za mwili wake.

No comments: