Tuesday, November 17, 2015

MTOTO ALIYEPIGWA KITU KIZITO KICHWANI MBINGA AMEFARIKI DUNIA



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MTOTO Moses Ndunguru (3) aliyekuwa akiishi na wazazi wake mtaa wa Tangi la Maji A Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambaye alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kukimbizwa Hospitali ya Misheni Peramiho wilaya ya Songea mkoani humo, amefariki dunia na kuzikwa leo katika makaburi ya Misheni yaliyopo mjini hapa.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela.
Aidha kufuatia ukatili huo aliofanyiwa mtoto huyo, wenzake wawili ambao nao walifanyiwa hivyo walifariki dunia papo hapo usiku wa Novemba 15 mwaka huu, na miili yao kuzikwa katika makaburi yaliyopo mtaa wa Misheni Mbinga mjini.

Watoto hao wawili ambao walipoteza maisha katika tukio hilo ni, Lulu Chang’a (14) na Furaha Ndunguru (7) ambaye ni wa darasa la kwanza shule ya msingi Nyerere iliyopo mjini hapa.


Aliyesababisha mauaji hayo ni mkazi mmoja wa kijiji cha Zomba wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Dickson Lupogo (28) ambaye naye baada ya kufanya hivyo alipigwa na watu wenye hasira kali, mwili wake kuchomwa moto na kupoteza maisha ambapo alizikwa katika kijiji hicho. 

Hata hivyo Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, ili kuweza kubaini chanzo chake.

No comments: