Saturday, November 14, 2015

MBINGA KUNUFAIKA NA MPANGO WAKALA WA MISITU NA NYUKI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, watanufaika na mpango uliowekwa na Wakala wa misitu na nyuki wilayani humo, wa kuwagawia mbegu za miti na kwenda kuotesha katika vitalu maalumu, ili baadaye iweze kupatikana miche ya miti ambayo itapandwa katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya hiyo.  

Vicent Mwafute.
Mpango huo, umekuwa ukitekelezwa kupitia vikundi ambavyo vimesajiliwa kisheria ambapo hupewa mbegu na kwenda kuzalisha miche ambayo baadaye husambazwa kwa wananchi, kwa ajili ya kwenda kuipanda katika mashamba yao.

Ofisa misitu wa wilaya hiyo, Vicent Mwafute alisema hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari juu ya suala la utunzaji wa mazingira na misitu wilayani Mbinga.

Alisema kuwa tayari kilo 120 za mbegu ya miti rafiki ya maji, zimenunuliwa na kupelekwa kwenye vikundi husika, ili waweze kuzalisha katika vitalu na baadaye isambazwe kwa wananchi tayari kwa kupanda.


“Hivi sasa uelewa umekuwa mkubwa kwa wananchi hapa wilayani juu ya umuhimu wa upandaji miti, mimi na wenzangu katika idara yetu tumekuwa tukijitahidi kuwahamasisha na sasa jambo hili lina mwitikio mkubwa”, alisema Mwafute.

Kadhalika aliongeza kuwa lengo la wilaya, katika kipindi hiki cha mwaka 2015/2016 ni kuzalisha miche milioni 3 na kuifikisha kwa wananchi, ili waweze kuipanda katika mashamba yao hasa  kipindi hiki cha kuelekea msimu wa mvua za masika.

Vilevile kwa upande wa udhibiti vitendo vya uchomaji moto, katika misitu iliyopo wilayani humo, Mwafute alisema ni changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo hasa kipindi cha kiangazi kutokana na baadhi ya watu kwa makusudi, wamekuwa wakiichoma moto pasipokuwa na sababu yoyote ile ya msingi. 

Alifafanua kuwa kufuatia hali hiyo, wananchi wanaendelea kuelimishwa waweze kuachana na tabia hiyo na kwamba Halmashauri ya wilaya ya Mbinga imekuwa ikiwasaka wahusika wa vitendo hivyo na kuwachukulia hatua za kisheria, ili iwe fundisho kwa wengine kwa lengo la kudhibiti visiweze kuendelea.

Zao la misitu katika Halmashauri hiyo ni la tatu katika kuwaingizia mapato hivyo kutokana na umuhimu huo wataalamu wa idara ya misitu na wadau mbalimbali, wamekuwa bega kwa bega kuhakikisha kwamba misitu inaendelezwa ipasavyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: