Sunday, November 22, 2015

WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KUGONGA MTAMBO WA KUJENGA BARABARA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU watatu wamefariki dunia katika ajali ya pikipiki, baada ya kugonga mtambo wa kujenga barabara (ROLA) ambao ni mali ya kampuni ya Sino Hydro inayojenga barabara kwa kiwango cha lami, kutoka Tunduru mjini kuelekea katika tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.

Mashuda wa tukio hilo, walisema kuwa  ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Muhuwesi wilayani humo ambapo Diwani wa kata ya Muhuwesi,  Nurdini Mnolela aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ajali hiyo ilitokea Novemba 15 mwaka huu wakati watu hao wakiwa wanatokea kijiji cha Majimaji kurejea kijijini kwao Muhuwesi.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, wa pikipiki waliyokuwa wakiendesha ambayo ni aina ya Sunlg yenye namba za usajili T 317 CUC mali ya  marehemu Ahamad Athuman (30) hali ambayo, ilimfanya ashindwe kuimudu na hatimaye kugonga mtambo huo.


Katika tuko hilo diwani huyo alisema, marehemu alikuwa amewabeba abiria wawili ambao wote nao walifariki dunia katika eneo la tukio ilipotokea ajali hiyo.

Mganga aliyefanyia uchunguzi miili ya marehemu hao, Dokta George Chiwangu alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo kilisababisha na kutokwa damu nyingi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Chiwangu alibainisha kuwa katika ajali hiyo marehemu wote, walipata majeraha vichwani jambo ambalo lilisababisha kupasuka vichwa vyao na ubongo kuvurugika.

Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha kuwepo kwa ajali hiyo na kuwatahadharisha madereva wa vyombo vya moto kuwa makini pindi wanapopita katika barabara, ambazo bado zipo katika matengenezo.

Hata hivyo alisema endapo kama hawatakuwa makini, wakati wanapoendesha vyombo hivyo, ipo hatari vijana wengi kuendelea kupoteza maisha na wengine kuwa walemavu wa maisha.

No comments: