Sunday, November 15, 2015

WATATU WAUAWA KIKATILI MBINGA MMOJA MWILI WAKE WACHOMWA MOTO


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mtu mmoja ambaye ni mkazi wa kijiji cha Zomba wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Dickson Lupogo (28) ameuawa kikatili kwa kushushiwa kipigo kikali na baadaye mwili wake kuchomwa moto na watu wenye hasira kali, baada ya kufanya mauaji ya watoto wawili na kumjeruhi mmoja.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela.
Mwandishi wa habari hizi ambaye aliwasili eneo la tukio, majira ya asubuhi leo Novemba 15 mwaka huu, alishuhudia mauaji hayo yaliyofanyika katika mtaa wa Tangi la maji A Mbinga mjini na kuelezwa kwamba, Lupogo alifanyiwa  unyama huo kutokana na kitendo chake cha kuwaua kikatili watoto hao na mmoja kumjeruhi vibaya.

Kadhalika Adrian Ndunguru ambaye ni mjomba wa Lupogo, alisema kuwa marahemu huyo alifanya mauaji hayo Januari 14 mwaka huu, majira ya usiku ambapo alienda nyumbani kwa Paulo Ndunguru katika mtaa huo wa Tangi la maji na kumweleza kwamba hawezi kurudi kijijini kwao Zomba, badala yake atalala hapo au ampeleke Polisi kwa maelezo kwamba akihofia atauawa endapo kama angerejea nyumbani kwake.


Adrian alifafanua kuwa baada ya kupokea maelezo hayo, Paulo hakukubaliana na wazo lake kwakuwa hakutoa ufafanuzi wa kina, badala yake alimwacha pale nyumbani na kwenda kwa mama yake marahemu Dickson Lupogo, anayeishi mtaa wa Masumuni jirani mjini hapa, kwa lengo la kushauriana naye juu ya maelezo hayo yaliyotolewa na mtoto wake.

Kwa upande wake akielezea tukio hilo, Paulo alisema kuwa wakati akiwa njiani kuelekea kwa dada yake, ghafla alipigiwa simu na mke wake Adella Mhagama akielezwa kwamba mjomba wake ambaye ni Lupogo, alikuwa akiwapiga watoto waliokuwa wamelala chumbani kwao.

Alisema baada ya kufika nyumbani kabla ya kuingia ndani alikutana na Dickson ambaye alimvamia ghafla huku akiwa ameshika kisu mkononi, na ndipo alipambana naye huku akipiga kelele akiomba msaada ambapo majirani waliwasili na kumkamata asiweze kuleta madhara, huku wakimfunga kamba miguu na mikono.

Baada ya tukio la kufungwa kamba, walipoingia ndani walikuta watoto watatu kati yao wawili wakiwa wameuawa na mmoja akiwa amejeruhiwa vibaya, pembeni yake pakiwa na chuma kizito chenye damu, ambacho kinadaiwa kutumika katika mauaji ya watoto hao.

Kugundulika kuuawa kwa watoto hao, ndiko kulizua hasira na walipotoka nje ndipo walimpiga vibaya mtuhumiwa aliyefanya ukatili huo wa kinyama na baadaye alichomwa moto majira ya saa 5:00 usiku, huku mwili wake ukiteketezwa baadhi ya maeneo.  

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja marehemu kuwa ni watoto wawili, Lulu Chang’a (14) na Furaha Ndunguru (7) ambaye ni wa darasa la kwanza shule ya msingi Nyerere iliyopo Mbinga mjini.

Msikhela alifafanua kuwa mtoto Moses Ndunguru (3) amejeruhiwa vibaya na amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, ambako anaendelea na matibabu na hali yake ni mbaya, na kwamba miili ya marehemu hao inatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao mjini hapa.

Pamoja na mambo mengine, Kamanda huyo wa Polisi aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ili kuweza kubaini chanzo chake na kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kuacha tabia ya kuchukua sheria mkononi badala yake watoe taarifa kwenye vymbo vya kisheria ikiwemo Polisi.

Hata hivyo Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Mbinga, Dokta Robert Elisha alisema kuwa miili ya marehemu hao imejeruhiwa vibaya kutokana na kupigwa na kitu kizito kichwani, kitendo ambacho kilisababisha kutokwa na damu nyingi na kwamba kwa upande wa mtoto aliyejeruhiwa, Moses Ndunguru ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na kwamba kutokana na hali yake kuwa mbaya, huenda akapelekwa Hospitali ya misheni Peramiho iliyopo wilaya ya Songea au Litembo hapa mkoani Ruvuma kwa matibabu zaidi.

No comments: