Sunday, November 29, 2015

CHAWATA MBINGA YA MUUNGA MKONO MAGUFULI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma kimesema, ifikapo siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu Desemba 3 mwaka huu wilaya ya Mbinga itafanya maadhimisho hayo, kwa kuwapatia walemavu wake mahitaji mbalimbali na sio kufanya sherehe kama ilivyozoeleka katika miaka iliyopita.

Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Martin Mbawala alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu juu ya mikakati ya kuwasaidia walemavu na kuwainua kutoka katika umaskini, ambao umekithiri miongoni mwao.

Alisema kuwa kufanya hivyo ni kuunga mkono agizo lililotolewa na Rais John Magufuli kwamba, hakuna sababu ya msingi ya watu kufanya sherehe ya kupika vyakula na kulipana posho kwa maadhimisho ya sherehe mbalimbali, bali fedha husika zikatumike katika shughuli za kimaendeleo.


“Ni vyema Chawata hapa Mbinga tukaweka maadhimisho yetu kwa mtindo huu, itakuwa sio busara kuliacha kundi hili tete litaabike kutafuta mahitaji muhimu kama vile fimbo nyeupe za kutembelea kwa watu wasioona, halafu tunatumia fedha nyingi kupika wali, kula nyama na kununua vinywaji ni vyema sasa fedha hizi zielekezwe kununua mahitaji maalum ya watu hawa”, alisema Mbawala.

Mbawala aliongeza kuwa chama hicho cha walemavu wilayani humo, katika kufanikisha hilo kimejiwekea pia mipango yake madhubuti ya kutafuta wahisani mbalimbali ambao wataweza kusaidia watu wenye ulemavu wilayani humo, kwa kuwapatia mahitaji maalum yatakayo wawezesha kusonga mbele katika maisha yao ya kila siku. 

Hata hivyo alifafanua kuwa walemavu wengi wilayani Mbinga, wanahitaji kusaidiwa baiskeli za kutembelea (Wheel chair), fimbo nyeupe, magongo, miwani na mafuta ya kupaka watu wenye matatizo ya ngozi (Albino).

No comments: