Wednesday, November 4, 2015

DED MADABA AWATAKA WATENDAJI KUWAJIBIKA KATIKA MAENEO YAO YA KAZI



Na Mwandishi wetu,
Madaba.

MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Robert Mageni amewataka watendaji wa vijiji, mitaa  na kata  katika wilaya hiyo kushughulikia matatizo ya wananchi katika maeneo yao ya kazi, na sio kuwaacha wakitaabika peke yao bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Mageni alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na  Madiwani wapya na Mbunge mteule wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti vya utambulisho pamoja na kupeana mikakati ya utekelezaji wa mipango mbalimbali  yenye lengo la kuongeza kasi ya maendeleo na ufanisi wa kuwatumikia wananchi, iliyofanyika mjini hapa.


Alisema jimbo hilo ni jipya, hivyo linahitaji viongozi waliochaguliwa kuwa na mshikamano  ili waweze  kuboresha huduma za kijamii, ambapo alitolea mfano kama vile ujenzi wa vyumba vya maabara kwa shule za sekondari.

Mkurugenzi huyo alisema, watendaji wa serikali hawapaswi kulalamika badala yake wao ndiyo wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na kuchukua hatua madhubuti, kumaliza kero za wananchi katika maeneo yao.

Aidha aliwataka watumishi hao kuwa na ushirikiano na madiwani walioteuliwa kuongoza kata zilizopo ndani ya wilaya ya Madaba, kwa kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaoharibu mazingira  ikiwemo ukataji miti na uchomaji misitu hovyo, ambao husababisha  kuharibu na kupungua kwa vyanzo vya maji.

No comments: