Sunday, November 22, 2015

MBINGA WAFANIKIWA AKINA MAMA WAJAWAZITO KUJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA



Na Muhidin Amri,
Mbinga.

WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, imefanikiwa kuongeza kiwango cha  akina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya na Hospitali, kutoka asilimia 76 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 90  mwezi Juni mwaka huu.

Mbali na hilo, pia kiwango cha wateja wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango nacho kimezidi kuongezeka, kwani hivi sasa idadi ya wazazi wanaopata huduma hiyo imefikia asilimia 105 kutoka asilimia 33, mwaka 2013 na asilimia 85 kwa mwaka 2014. 

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga.
Hayo yamebainishwa  na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa akizungumza  na mwandishi wa habari hizi juu ya kuimarika kwa huduma ya akina mama wajawazito wilayani humo na mkakati wa kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya ukimwi (VVU)  kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kabla na baada ya kujifungua. 

Ngaga alisema, idadi ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kutoka vifo  169 sawa na vifo 10/1000 mwaka 2013 hadi kufikia vifo 84 ambavyo ni sawa na vifo 7/1000 na mpango uliopo ni kumaliza kabisa vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua akina mama hao, kwani baadhi yake vinatokana na uzembe wa mama kushindwa kuwahi hospitali mapema. 


Aidha Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alibainisha kwamba wilaya yake imefanikiwa kupunguza kiwango cha vifo vya mama wajawazito/wazazi kutoka (11)65/100,000 mwaka 2013 hadi kufikia (8)61/100,000 mwaka 2014 hata hivyo bado wanaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo hilo na dhamira yao ni kupunguza, hadi kufikia wastani wa vifo (4)35/100,000. 

Katika mkakati huo alisema unakwenda sambamba na suala la kutoa elimu   juu ya ukimwi, pamoja na kuwapima akina mama wanaokwenda katika zahanati, vituo vya afya na hospitali  kufuata huduma za uzazi kikamilifu, ambapo akina mama 6,810 waliojifungua, kati yao 591 waligundulika kuwa na matatizo kabla na baada ya kujifungua. 

Ngaga alisema, akina mama 5,219 ambayo ni sawa na asilimia 76.6 walijifungua kwa njia ya kawaida na 1,214 walijifungua kwa njia ya upasuaji na waliopata huduma za dharura zinazotolewa katika vituo vitano na kati yao akina mama  6,047 waliojifungua waliingia chumba cha uzazi wakiwa wamepimwa.

Hata hivyo alieleza kuwa mpango huo tayari kuna vituo 59, vinavyotoa huduma ya chanjo kwa watoto na watoto 5,966 walipata chanjo ya penta 3 kati yao watoto 184 walizaliwa na akina mama wenye virusi vya ukimwi na 179 waliochukuliwa damu kwa ajili ya uchunguzi, watoto sita waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

No comments: