Sunday, November 22, 2015

WATOTO WATEKETEA MOTO BAADA YA MAMA YAO KUWAFUNGIA NDANI YA NYUMBA



Na Steven Augustino,
Songea.

WATU watatu wamefariki dunia, katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika kijiji cha Madaba kata ya Mahanje wilaya ya Songea na kata ya Makambi Manispaa ya Songea, hapa mkoani Ruvuma.

Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mihayo Msikhela alisema kuwa matukio yote yalitokea November 16 mwaka huu na kwamba tukio la kwanza lilitokea kijiji cha Madaba, kata ya Mahanje ambapo watoto wawili walikutwa wakiwa wameungua moto na miili yao kuteketea kabisa.

Mihayo Msikhela, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma.
Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa tukio hilo la watoto kuungua moto, lilisababishwa na mshumaa ambao waliwashiwa na mama yao mzazi ambaye wakati tukio hilo linatokea alikuwa kwenye sherehe za kushangilia ushindi wa Diwani wa kata Mahanje, Stephano Mahundi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliofanyika November 16 mwaka huu.

Msikhela aliwajata marehemu hao kuwa ni, Happy Mgani (4) na Chesco Mhagama (2) na kwamba mama huyo ambaye hakutaka kumtaja jina lake, yupo chini ya ulinzi wa Polisi kwa mahojiano zaidi.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, mama huyo aliwafungia kwa nje watoto hao na kwenda kwenye sherehe hizo  ambapo hadi moto huo unawaka,  majira ya saa 8 za usiku alikuwa bado hajarejea nyumbani kwake.

Aidha Kamanda Msikhela alilitaja tukio jingine kuwa lilitokea katika kata ya Makambi Manispaa ya Songea kwamba, mtu aliyefahamika kwa jina la Ngaponda Khalifa (25) alifariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali, baada ya kumchoma kisu mpenzi wake aliyefahamika kwa jina la Hawa Swaleh (18).

Alisema katika tukio hilo Marehemu Khalifa alikwenda kwa mwanamke huyo, kwa lengo la kumuomba radhi na kumtaka warudiane na kuishi kama mume na mke na kwamba alichukua maamuzi ya kumchoma kisu, baada ya ombi lake kukataliwa.

Majeruhi Hawa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ligela, amelazwa Hospitali ya mkoa wa Ruvuma (HOMSO) kwa matibabu zaidi na akaongeza kuwa Polisi wamejipanga kufanya oparesheni ya kuwanasa waliohusika katika tukio hilo, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

No comments: