Wednesday, November 4, 2015

NALICHO NAMTUMBO AKEMEA WANAOHUJUMU MIUNDOMBINU YA BARABARA



Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho amekemea tabia ya baadhi ya watu wasiojulikana kuhujumu miradi  ya barabara  ikiwemo kung’oa alama za barabarani, ambazo husaidia watumiaji kutambua vizuri wanapokuwa barabarani  na kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Nalicho ametoa kauli hiyo kufuatia kuwepo kwa baadhi ya watu, kuanza kuharibu alama zilizowekwa barabarani katika barabara mpya ya Namtumbo  hadi Songea ambayo ujenzi wake, umekamilika na kuanza kutumika.

Alisema kuwa licha ya uharibifu huo unaofanywa na watu hao, wamekuwa pia wakiiba baadhi ya vifaa kama vile mabomba na alama nyingine ambazo husaidia watumiaji wake kutambua na kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani, jambo ambalo husaidia kupunguza kiwango cha ajali hasa kwa watembea kwa miguu.


Kadhalika alieleza kuwa ni vyema watanzania wakawa na tabia ya kuthamini na kutunza miradi yao, ambayo serikali hutumia fedha nyingi kuijenga kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake.
 
“Ninachowataka hapa wananchi watunze miradi hii ya maendeleo katika wilaya yetu, serikali inatumia gharama kubwa kuijenga kwa manufaa yetu sisi wananchi kwa kizazi cha sasa na kijacho”, alisema Nalicho.

No comments: