Friday, November 20, 2015

MAHANJE CCM WAIBUKA KIDEDEA

Na Muhidin Amri,
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimeibuka kidedea baada ya mgombea wake wa udiwani katika Kata ya Mahanje jimbo la Madaba wilayani humo, Stephano Mahundi kufanikiwa kushinda katika kiti hicho baada ya kumshinda mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hans Mlelwa.

Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika mwezi uliopita, baada ya kukosekana kwa karatatsi za kupigia kura kwa nafasi ya udiwani, hata hivyo katika nafasi ya ubunge na rais uchaguzi uliendelea kama uilivyopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi kata ya Mahanje, Kanisius Lingowe alimtangaza mgombea huyo wa CCM kuwa mshindi baada ya kufanikiwa kupata kura 946, dhidi ya mgombea wa CHADEMA Hans Mlelwa aliyeambulia kura 487 ambaye hata hivyo, hakuwepo katika chumba cha kutangaza matokeo hayo.


Lingowe alifafanua kuwa, katika kata hiyo jumla ya wananchi waliojiandikisha walikuwa 12,325 waliojitokeza kupiga kura ni 1,449 huku kura halali zilikuwa 1,433 na kwamba zilizoharibika kulikuwa na kura 16.

Kwa mujibu wa msimamizi huyo wa uchaguzi, alisema sheria ya Tume ya taifa ya uchaguzi inayo mamlaka ya kutangaza matokeo ya kura zilizopigwa na kumtangaza mshindi, hata kama wagombea hawatakuwepo eneo husika na tume itakachofanya ni kuwapa taarifa wagombea hao.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mahundi ameahidi kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata hiyo sambamba na kuwatumikia kikamilifu wakazi wa Mahanje, ikiwemo  namna ya kuboresha huduma za kijamii kama vile afya, maji, elimu na miundombinu kwa baadhi ya maeneo.

Mahundi alisema, jambo la kwanza atakalolipa kipaumbele ni kuhakikisha wakazi wa kata hiyo wanakuwa na shughuli za kufanya ili kujipatia kipato halali na kukomesha tabia ya kukaa vijiweni kwa muda mrefu, jambo linalochangia umaskini licha ya ukweli kwamba, kuna rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

Aidha, ameahidi kushirikiana na serikali, wataalamu wake waliopo na wadau wengine wa maendeleo kuanzisha vikundi mbalimbali vya ujasiriamali, kama vile wanawake na makundi ya vijana ili waweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira ambao umekuwa kama wimbo kwa makundi hayo hapa nchini.

Mbali na hilo, Mahundi alisema atatoa ushirikiano kwa  vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kata hiyo na jimbo lote la Madaba, kunakuwa na amani na utulivu ili kutoa nafasi kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi badala ya kutumia muda wao kutafuta suluhu ya migogoro, kitendo ambacho kinaweza kurudisha  nyuma maendeleo ya wananchi.


Kutokana na hali hiyo, diwani huyo mteule amewataka wakazi wa kata hiyo akiwemo aliyekuwa mshindani wake kisiasa kumpatia ushirikiano wa kutosha katika majukumu yake mapya, ili aweze kutekeleza ahadi zote alizotoa kwa wananchi badala ya kuendelea kununiana, kwani tayari uchaguzi umekwisha na kwamba kuna maisha mbele ambayo wananchi wanahitaji maendeleo.

No comments: