Friday, November 6, 2015

MBINGA KWAFUKUTA NAFASI YA MWENYEKITI HALMASHAURI YA MJI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KAMPENI za chini kwa chini zinaendelea kufukuta katika Jimbo la Mbinga mjini, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambazo zinalenga kumpata Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga atakayeweza kuendesha baraza la madiwani la halmashauri hiyo. 

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa, baadhi ya Madiwani waliochaguliwa katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu wameanza kuvutana hapa na pale, juu ya kumpata mwenzao atakayeweza kuendesha gurudumu hilo katika baraza lao.


Vikao vya siri vimekuwa vikifanyika katika maeneo mbalimbali, ambapo baraza hilo kwa kiasi kikubwa lina madiwani wengi, ambao ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Halmashauri ya mji huo imeundwa na kata 19 ambapo katika kata hizo, mbili zinaongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa nafasi hiyo ya udiwani.

Duru za kisiasa ambazo zimetufikia mezani na kuthibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari zinayataja majina mawili, (ambayo tunayo) yanavutana kutaka kushika nafasi hiyo ya uenyekiti.

Hata hivyo nimezungumza na wadau wa mambo ya kisiasa wilayani Mbinga, walisema kwa nyakati tofauti kwamba licha ya kuwepo kwa mvutano huo, bado kuna madiwani wengine ambao watajitokeza baadaye kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, huku wakiongeza kuwa hawataki kujitokeza sasa ni mapema mno.

…………. itaendelea wiki ijayo.

No comments: