Sunday, November 15, 2015

WAWILI WAFARIKI DUNIA TUNDURU KATIKA MATUKIO TOFAUTI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MOHAMED Layi (29) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Namiungo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, amefariki dunia baada ya nyumba yake aliyokuwa akiishi huku akiwa amelala kuchomwa moto, na watu wasiofahamika.

Tukio lilitokea majira ya usiku Novemba 12 mwaka huu, baada ya kufungiwa kwa kufuli nje ya nyumba yake na watu hao.

Akizungumza kwa taabu kabla ya kufariki dunia marehemu, Mohamed ambaye alikimbizwa katika Hospitali ya wilaya hiyo kwa matibabu zaidi alisema kwamba  kabla ya kukumbwa na mkasa huo, alisikia sauti za watu wawili wakizungumza nje ya nyumba yake.


“Ghafla niliona mwanga mkubwa wa moto jambo ambalo, lilinifanya nipige kelele kuomba msaada lakini sikuweza kupata msaada”, alisema. 

Katika tukio la pili ambalo lilitokea kitongoji cha Matawala kilichopo kijiji cha Mtonya, David Ernest  naye alifariki dunia  baada ya kuchomwa kisu na mjomba wake.
Chanzo cha ugomvi huo kilitokana na ulevi wa pombe za kienyeji, ambazo walikuwa wamekunywa kupita kiasi, aina ya gongo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha juu ya mauaji hayo na kwamba mtuhumiwa wa tukio hilo la pili, Filemon Kauleta (64) tayari amekamatwa ambapo kwa tukio la pili uchunguzi unaendelea kufanyika.

Vilevile Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru, Dokta Gaofrid Mvile alisema, marehemu Layi alipoteza maisha kutokana na  mwili wake kuungua vibaya.

Kuhusu kifo cha Ernest, mganga huyo alisema alifikwa na umauti kutokana na kutokwa na damu nyingi iliyosababisha damu kuchanganyika na ubongo, baada ya kuchomwa kisu hicho.

No comments: