Saturday, November 14, 2015

UJENZI WA MRADI MBINGA WAKAWAMA MKAKO NA LITOHO WAKOSA MAJI SAFI NA SALAMA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Mkako na Litoho, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, hawana maji safi na salama kutokana na serikali kushindwa kukamilisha ujenzi wa miradi miwili ya maji, iliyopo katika vijiji hivyo.

Aidha hali hiyo, imesababishwa na ukosefu wa fedha shilingi bilioni 1,082,199,509 ambazo mpaka sasa serikali haijazipeleka katika maeneo hayo, kwa ajili ya kuweza kufanya kazi ya ujenzi wa miradi hiyo.

Mhandisi wa maji wilaya ya Mbinga, Vivian Mndolwa alibainisha kwamba mkandarasi husika ambaye alipewa miradi hiyo kwa ajili ya ujenzi, amefikia kiwango cha asilimia 60 cha ujenzi na sasa imesimama kutokana na ukosefu huo wa fedha.


“Hii miradi ni mikubwa na fedha tunategemea kupata kutoka kwa wafadhili, hivyo imekwama ujenzi wake kutokana na sababu hiyo, hivyo tunaiomba serikali ione namna gani ya kumaliza jambo hili”, alisema Vivian.

Vivian alifafanua kuwa ujenzi wa miradi hiyo hapo ulipofikia, kiasi kikubwa cha fedha zilizotumika katika ujenzi wake zimetoka kwa mkandarasi aliyepewa mradi na kwamba hivi sasa, anaidai serikali shilingi milioni 932,746,483 ili aweze kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo.

Pamoja na mambo mengine, Mhandisi huyo wa wilaya ya Mbinga, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutunza vyanzo vya maji hasa katika maeneo ambayo miradi ya maji, ujenzi wake umekamilika.

Alisema waache vitendo vya uharibifu wa misitu na wizi wa mabomba ya maji ambayo yamefukiwa chini ya ardhi, kwani vitendo vya kuhujumu miundombinu ya maji kunahatarisha ustawi wa maendeleo yao katika jamii.

“Licha ya kukamilika kwa baadhi ya miradi ndani ya wilaya yetu, wapo baadhi ya wananchi wanakiburi, wamekuwa wakilima mashamba karibu na vyanzo vya maji jambo ambalo ni la uharibifu wa mazingira”, alisema.

Kufuatia uharibifu huo ambao unafanywa na watu wachache, aliongeza kwamba idara imekuwa ikichukua hatua kwa kuwaandikia barua za onyo uongozi husika wa kijiji, ikiwa ni lengo la kuwataka wahame wasiendelee kufanya uharibifu huo.

Vivian alieleza pia, elimu imekuwa ikitolewa kwa wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo hivyo ili viweze kuwa endelevu na kuzalisha maji wakati wote, na walaji waweze kuondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama.

No comments: