Monday, November 2, 2015

MADIWANI NA WABUNGE WATEULE MBINGA WATAKIWA KUSIMAMIA MAENDELEO


Na Steven Augustino,

Mbinga.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga  mkoani Ruvuma, kimewataka madiwani na wabunge wateule kufanya kazi za kuwatumikia wananchi,  ili kuondokana na tatizo la umaskini unaoendelea kutafuna wananchi wa wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa na Katibu wa CCM wa wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa alipokuwa akizungumza na viongozi hao wateule na baadhi ya wanachama wa Chama hicho kwenye sherehe fupi ya kuwapongeza iliyofanyika ukumbi wa Mbicu hotel uliopo mjini hapa.

Alisema yeye kama mtendaji mkuu wa chama ngazi ya wilaya, amefurahishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu yameonesha bado chama hicho kinapendwa na wananchi, tofauti na baadhi ya watu wengine wanavyofikiri.


Kwa mujibu wa Katibu huyo, alisema kuwa wagombea wa CCM wamepata ushindi ambao yeye binafsi hakutegemea kutokana na upinzani mkubwa uliokuwepo hasa katika jimbo la Mbinga mjini, ambapo wagombea wa vyama vingine  kama vile NCCR Mageuzi walikuwa wakitumia ukabila kutaka kumchafua mgombea wa CCM asiweze kupata ushindi katika uchaguzi huo.

Aliongeza kuwa hata katika nafasi ya udiwani chama hicho, kimeweza kushinda viti vingi zaidi ikilinganishwa na vyama vingine, na kwamba jimbo la Mbinga mjini kulikuwa na wagombea 19 wa udiwani ambapo CCM imeshinda viti 17 huku Chadema ikiambulia viti 2.

Alisema atika jimbo la Mbinga vijijini, kulikuwa na kata 29 katika matokeo ya uchaguzi huo, CCM bado  kimeendelea kufanya vizuri baada ya madiwani wake, 28 kuchaguliwa kuingia katika baraza la madiwani la mwaka 2015/2020 na CHADEMA kikipata diwani mmoja tu.

Alifafanua kuwa, hata kwa nafasi ya urais mgombea wa CCM amemshinda kwa kura nyingi  mgombea wa CHADEMA ambapo katika kata 48 zilizopo wilayani humo, Dokta  John Magufuli ameshinda kata 47 na Edward Lowassa akiambulia ushindi katika kata moja ya Mbinga mjini B.

Mbali  na ushindi huo, mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Mbinga mjini mwandishi wa habari gazeti la Uhuru mkoani Ruvuma, Dastan Ndunguru aliibuka mshindi baada ya kupita bila kupingwa katika kata ya Kihungu.

No comments: