Sunday, November 15, 2015

SERIKALI YAOMBWA KUJENGA JENGO LA MAABARA MBINGA


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SERIKALI hapa nchini, imeombwa kujenga jengo jipya la kitengo cha maabara katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kutokana na jengo linalotumika sasa, halitoshelezi mahitaji husika.

Aidha kitengo hicho hivi sasa, kinakabiliwa na mapungufu ya vitendea kazi ikiwemo vifaa tiba na dawa jambo ambalo husababisha wataalamu wa maabara katika hospitali hiyo, wakati mwingine kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

John Chihapula ambaye ni Mkuu wa kitengo cha maabara wilayani Mbinga, alisema hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ambao walitembelea hospitalini hapo, kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.


“Jitihada za makusudi inapaswa zichukuliwe ili kuweza kunusuru hali hii isiweze kuendelea, jengo letu la maabara limekuwa finyu halitoshelezi mahitaji tunahitaji serikali ijenge jengo lingine kubwa, ambalo litakidhi mahitaji ya utendaji wa kazi zetu za kila siku”, alisema Chihapula.

Chihapula alifafanua kuwa, hata wagonjwa wamekuwa wakipata shida kutokana na jengo hilo kukosa sehemu ya kupumzikia, wakati wanaposubiri majibu yao ya vipimo vya magonjwa badala yake hulazimika kusimama nje ya jengo kwa muda mrefu.

Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa vifaa tiba, serikali imekuwa ikifanya jitihada ya kutafuta vifaa hivyo kutoka kwa wafadhili mbalimbali.

Alisema kufuatia kuwepo kwa jitihada hizo, hivi sasa Hospitali ya wilaya ya Mbinga imepata mashine mpya ya kisasa, Gin Expert na Darubini moja ambavyo hutumika kupimia magonjwa ya kifua kikuu na kwamba wakati wowote itaanza kufanya kazi, baada ya taratibu husika kukamilika. 

Mkuu huyo wa kitengo cha maabara wilayani humo, aliongeza kuwa kutokana na hospitali kila siku hupokea wagonjwa wengi zaidi ya 200 wa matibabu ya ndani na nje, kuna kila sababu ya kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa kuwa na vifaa tiba na dawa vinavyojitosheleza, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima miongoni mwa jamii.

No comments: