Friday, November 20, 2015

RUVUMA WAPONGEZA UTEUZI WA KASSIM MAJALIWA KUWA WAZIRI MKUU

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Muhidin Amri,
Songea.

BAADHI ya wananchi katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamefurahishwa na uteuzi wa Mbuge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa kuwa Waziri mkuu wa Tanzania, katika serikali hii ya awamu ya tano.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini hapa, walisema kuwa Majaliwa ndiye mtu sahihi anayefaa  kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wa kazi zake alipokuwa Naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu.

Mmoja wa wakazi hao, Thomas Komba alisema ni mtu ambaye ataendana na kasi ya Rais Magufuli lakini pia wakati wote amekuwa kiongozi mwadilifu na mchakapakazi hodari, ambaye hana makundi.


Dokta Magufuli katika utendaji wake wa kazi, alioonesha  tangu alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza siku chache zilizopita alidhihirisha wazi kwamba serikali yake inahitaji watu makini ambao sio wazembe, katika kuamua mambo mbalimbali ya maendeleo  ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mariam Yusuf, mkazi wa mtaa wa Misufini kata ya Misufini mjini Songea alisema kuteuliwa kwa Majaliwa kuwa Waziri mkuu ni ishara tosha kwamba serikali ya awamu ya tano, ni watu wa ‘hapa kazi tu’ ambao wanahitaji kuwatumikia Watanzania ipasavyo.

"Kwa kweli mimi nikiwa mfuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) sasa nina imani na serikali hii ya Dokta Magufuli, hata huyu aliyetangazwa kushika nafasi ya Waziri mkuu ni mtu sahihi anayetambua majukumu yake ya kila siku, tutamuunga mkono katika utekelezaji wa maendeleo ya wananchi”, alisema Mariam.

Nao baadhi  ya waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, hawakubaki nyuma kuonesha imani yao kwa Majaliwa ambapo Julius Konala  licha ya kumpongeza Waziri huyo amewataka Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao kumuunga mkono, katika utumishi wake wote ili kumsaidia Rais Magufuli katika mapambano dhidi ya vitendo viovu, vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya watumishi wa umma hapa nchini.

Alisema, Dokta Magufuli na Majaliwa ni viongozi makini ambao wataweza kuivusha nchi yetu katika mapambano dhidi ya rushwa, dhuluma na wizi ambavyo vilisababisha hata wananchi kukata tamaa na kushindwa kuunga mkono mambo ya kimaendeleo.

Naye Cresensia Kapinga mbali na kukunwa na uteuzi huo, amewaomba viongozi wengine watakaoteuliwa katika serikali ya awamu ya tano kuwa watu wanaowajibika katika majukumju yao ya kila siku, busara na uaminifu.

Aliongeza kwamba, kwa imani aliyonayo ni dhahiri kuwa  viongozi hao wawili ndiyo watakaorudisha heshima ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani baadhi ya wananchi walitofautiana kwa kile alichoeleza kuwepo kwa baadhi ya watu ndani ya serikali, kutokuwa na uwezo katika utendaji wa shughuli za kila siku.

No comments: